TFRA YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO SHAMBA LA SUMRY RUKWA
Ikiadhimisha Siku ya Mbolea Duniani, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Joel Laurent, imefanya ziara ya mafunzo katika Shamba la Sumry (Msipazi Farm), kwa lengo la kujifunza teknolojia mpya za kilimo zinazoongeza uzalishaji na tija.
Ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 13, 2026, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa ambapo washiriki wamepata fursa ya kujifunza teknolojia mpya za kilimo cha biashara.
Akizungumza na ujumbe huo, Salum Sumry amesisitiza umuhimu wa kupima afya ya udongo ambapo matokeo yake yatakuongoza kuamua aina ya virutubisho vinavyohitajika na udongo na zao.
Kupitia ziara hiyo, TFRA imesisitiza umuhimu wa wakulima kutumia mbolea bora kwa kuzingatia aina ya zao, hatua ya ukuaji na hali ya udongo, pamoja na matumizi sahihi ya pembejeo ili kuongeza mavuno na kupunguza gharama zisizo za lazima.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Mamlaka kuimarisha uelewa wa wakulima na wadau kuhusu fursa zilizopo katika tasnia ya mbolea, hususan kwa vijana na wanawake, ili kuchochea ubunifu na maendeleo endelevu ya kilimo nchini.
