Ofisi ya Rais, Maendeleo ya vijana, yawatambua wadau wa mbolea
Serikali kupitia Ofisi ya Raisi, Maendeleo ya Vijana imewatambua na kuwatunuku tuzo wadau wa mbolea vijana walioonesha ubunifu katika kukuza tasnia ya mbolea nchini na kuwezesha vijana wengi kujikwamua kiuchumi na kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana.
Hayo yamebainishwa tarehe 12 Oktoba, 2026 wakati wa hafla za kilele cha Kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Nazareth Sumbawanga mkoani Rukwa kuelekea kilele cha mbio za Mwenge.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo ya Wakala Bora Kijana wa Usambazaji wa Mbolea, Oraph Stanley Mhema, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mhema Agrovert Limited, amesema alianza biashara ya mbolea miaka kumi iliyopita kwa mtaji wa shilingi 600,000. Amesema kuwa tangu wakati huo, biashara yake imeendelea kukua na kufikia mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 100.
Mhema amesema kuwa hadi sasa amesajili mawakala vijana zaidi ya 300, huku akilenga kuongeza idadi hiyo hadi kufikia 600. Amesema mawakala hao watasaidia kusogeza pembejeo karibu na wakulima, kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kuzifuata na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo ndani ya umbali usiozidi kilomita tano (5).
Kwa upande wake Mbunifu wa Mfumo wa kidijitali wa pembejeo za ruzuku, Mahmoud Shoo ameeleza nia yake ya kuendelea kuongeza juhudi katika kujenga mifumo ya kidijitali ili kuweza kurahisisha upatikanaji wa takwimu na kuiwezesha serikali kuweka na kupima ufikiwaji wa malengo iliyojiwekea katika kuhudumia wananchi.
Naye David Denis, mbunifu na mwanzilishi wa Kampuni ya Cuttoff Recycle Limited, aliyetunukiwa tuzo ya kutambua mchango na ubunifu wa vijana katika uzalishaji wa mbolea, amewataka vijana kutumia changamoto zilizopo katika maeneo yao kama fursa za kujiajiri, kujipatia kipato na kukuza uchumi wao.
