TAARIFA KWA UMMA: BEI ELEKEZI KWA MBOLEA ZA DAP, CAN, PANDA POWER NA YARAVERA AMIDAS KWA MSIMU WA KILIMO 2026/2027 (Toleo la 26)
Septemba 29, 2026
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inajukumu la kutoa bei elekezi kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea Na. 9 ya Mwaka 2009 na Kanuni ya 42 ya Kanuni za Mbolea za Mwaka 2026. Katika kutekeleza jukumu lake la kisheria, TFRA imefanya mapitio ya bei elekezi kwa mbolea za DAP, CAN, Panda Power na Yaravera Amidas zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Bei hizo zinapatikana kwenye tovuti ya TFRA kupitia anuani ya TFRA | Bei Elekezi za Mbolea 2026 na kwenye Mfumo wa Ruzuku ya Mpembejeo za Kilimo kwa wafanyabiashara. Bei hizi zitaanza kutumika tarehe 30 Septemba, 2026. Lengo la kufanya mapitio na kutangaza bei elekezi ni kuhakikisha kuwa mbolea inauzwa kwa bei inayoendana na gharama halisi za soko. Wafanyabiashara wa mbolea wanatakiwa kuuza mbolea hizo kwa bei elekezi au chini yake.
1. MJENGEKO WA BEI ELEKEZI
Bei elekezi zimezingatia gharama za manunuzi kutoka kwenye chanzo, usafirishaji na bima hadi kuifikisha nchini, gharama ya kubadilisha fedha, uondoshaji wa shehena bandarini, tozo za Mamlaka za Serikali, ufungashaji, usambazaji ndani ya nchi pamoja na faida za wafanyabiashara.
2. UUZAJI WA MBOLEA KWA WAKULIMA KUPITIA MFUMO
Katika msimu wa 2026/27 mbolea itaendelea kuuzwa kwa wakulima kupitia Mfumo wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo na kwa mujibu wa Mwongozo wa Ruzuku. Aidha, hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuuza mbolea nje ya mfumo isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka TFRA.
3. USIMAMIZI WA BEI ELEKEZI
Kwakuwa mbolea zote zinauzwa kupitia mfumo ni muhimu kwa Mamlaka zote husika katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa kila duka la pembejeo linabandika namba ya uwakala na bei elekezi sehemu za wazi na zinazoonekana kwa wanunuzi. Pia ni vema Mamlaka hizo zikasimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea. Aidha, tunatoa wito kwa wakulima na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa kwa Serikali mara tu wanapobaini vitendo vya ukiukwaji wa maelekezo kuhusu uzingatiaji wa bei elekezi na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima katika maeneo husika.
4. HITIMISHO
Serikali kupitia Mpango wa Ruzuku ya Mbolea inalenga kuwezesha wakulima kutumia mbolea zaidi ili kuongeza uzalishaji na tija na kuimarisha usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwanda na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Hivyo, Mamlaka inawasihi wataalam na wadau wa kilimo kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo. Aidha, TFRA inatoa wito kwa Mamlaka zote katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kutoa ushirikiano katika usimamizi wa mpango wa ruzuku ili Serikali ifikie azma yake na mkulima aweze kutumia fursa hii kuongeza tija katika uzalishaji kupitia kilimo.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI
MAMLAKA YA UDHIBITI WA MBOLEA TANZANIA (TFRA)
