TFRA YAITAMBUA KAMPUNI YA KUZALISHA MBOLEA ASILIA YA MABWEPANDE COMPOST
Kampuni ya Mabwepande Compost Management Limited ya jijini Dar es Salaam imepokea tuzo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kutambua mchango wake katika ubunifu na matumizi ya taka zinazooza kama malighafi ya kuzalisha mbolea ya mboji.
Hatua hiyo ni sehemu ya kutambua juhudi za kampuni hiyo katika kuongeza thamani ya taka, kuendeleza uzalishaji wa mbolea asilia na kuchangia utunzaji wa mazingira kupitia matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo.
Akikabidhi tuzo hiyo leo tarehe 17 Oktoba, 2026 katika makao makuu ya kampuni hiyo Bunju jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Louis Kasera amesema, tuzo hiyo inalenga kutambua na kuthamini mchango wa kibunifu wa kampuni hiyo kwa kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea za asili na kuunga mkono juhudi za kuendeleza tasnia ya mbolea nchini.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Uzalishaji kutoka Kampuni ya Mabwepande Compost Management Limited, Jimson Mkenda ameishukuru Mamlaka kwa kutambua mchango wao na kuitaja tuzo hiyo kuwa ni motisha ya kuendelea kuzalisha mbolea inayokidhi viwango vya ubora na kuwasaidia wakulima kupata mazao bora na yenye tija.
Nae, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TFRA, Daniel Maarifa amesema, mbolea za asili zinazozalishwa na viwanda vya ndani zinapaswa kupewa kipaumbele, huku akiwahimiza wadau kutembelea kiwanda hicho kujifunza mchakato wa uzalishaji na kuchangia kuongeza viwanda vya kuzalisha mbolea nchini.
Hatua hiyo ni juhudi za TFRA kutambua ubunifu katika uzalishaji wa mbolea za asili, kuhamasisha uwekezaji katika tasnia hiyo na kuhimiza matumizi bora ya taka zinazooza kwa kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya Sekta ya kilimo nchini.
