Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA na ZESCO waingia makubaliano kuimarisha uzalishaji wa mbolea ya mwani Zanzibar
13 Aug, 2026
TFRA na ZESCO waingia makubaliano kuimarisha uzalishaji wa mbolea ya mwani Zanzibar

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZESCO) wameingia makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuhakikisha uzalishaji wa mbolea inayotokana na mwani unakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Makubaliano hayo yameingiwa leo, Agosti 12, 2026, wakati wa Kongamano la Uchumi wa Blue lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kwanza Kizimkazi, Zanzibar.

Akizungumza katika kongamano hilo, 
Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA ameeleza kuwa, kama Mamlaka yenye jukumu la kudhibiti mnyororo mzima wa thamani wa mbolea, itahakikisha bidhaa hiyo inapitia hatua zote muhimu za uhakiki, upimaji na usajili kwa mujibu wa taratibu na viwango vilivyowekwa.

“Makubaliano tunayoingia leo yanalenga kuhakikisha tunakuza tasnia ya mbolea na sekta ya kilimo, kwa kuhakikisha tija ya uzalishaji inaongezeka kupitia matumizi sahihi ya pembejeo, huku mbolea ikiwa ni mojawapo ya pembejeo muhimu,” ameeleza Laurent.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ZESCO  Dkt Masoud Rashid Mohd amesemq Serikali kupitia Wizara inayohusika na Uchumi wa Blue inaendelea na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mwani ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji ndani ya miezi mitatu ijayo.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha mbolea inayotokana na mwani, huku uzinduzi rasmi ukitarajiwa kufanyika wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru.

Kupitia makubaliano hayo, TFRA na ZASCO watashirikiana katika kuhakikisha mbolea itakayozalishwa inafikia viwango vinavyotakiwa, pamoja na kufanya majaribio na tathmini ya ubora wa mbolea hiyo kabla ya kuanza kutumika kwa kiwango kikubwa.

Ushirikiano huo unatajwa kuwa ni hatua muhimu katika kuunganisha sekta ya Uchumi wa Blue na kilimo, hususan katika kuongeza thamani ya mwani na kuzalisha bidhaa zitakazoweza kuwasaidia wakulima kuongeza tija.