MAONESHO YA MBOLEA ASILI ZANZIBAR: DKT MWINYI ATEMBELEA BANDA LA TFRA
MAONESHO YA MBOLEA ASILI ZANZIBAR: DKT MWINYI ATEMBELEA BANDA LA TFRA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo tarehe 26 Septemba 2026 ametembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika Maonesho ya Tatu ya Zanzibar Organic Festival yanayofanyika Dole, Zanzibar, ambapo ameelezwa kuhusu juhudi zinazofanywa na Mamlaka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza kilimo hai.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema ushiriki wa Mamlaka katika maonesho hayo umefanyika kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Kilimo Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa buluu.
Amesema TFRA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha uzalishaji na matumizi ya mbolea yanafanyika kwa kuzingatia viwango na taratibu zilizowekwa, huku jitihada zikielekezwa katika kuongeza uzalishaji wa ndani na thamani ya mazao.
Aidha, TFRA pia imekuwa ikishirikiana na Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO), ambapo ushirikiano huo unalenga kuhakikisha bidhaa zinazotokana na mwani, ikiwemo mbolea, zinazalishwa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Akieleza kuhusu ushirikiano huo, Mtendaji Mkuu wa ZASCO, Dkt. Rashid Masoud Mohd, amesema ZASCO na TFRA wameendelea na makubaliano ya kuhakikisha uzalishaji wa mwani na bidhaa zake unakidhi viwango vinavyotakiwa, huku mbolea inayozalishwa ikiwa tayari imesajiliwa kwa mujibu wa taratibu.
Dkt. Rashid amesema ushirikiano huo umeendelea kusaidia kusukuma bidhaa hiyo kuelekea katika soko, pamoja na kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuongeza thamani ya zao la mwani, hatua inayochangia katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa nchi.
Katika kile kilichoonesha kuthamini mchango wa wadau katika kufanikisha maonesho hayo, TFRA imepewa tuzo na Rais wa Zanzibar tarehe 23 Septemba 2026, ikiwa ni kutambuliwa kwa Mamlaka kama mmoja wa wadau na wafadhili wa Maonesho ya Tatu ya Zanzibar Organic Festival.
Maonesho ya Tatu ya Zanzibar Organic Festival yanafanyika kuanzia Septemba 21 hadi 27, 2026, yakiwa na kauli mbiu isemayo “Fikiri kiulimwengu, Kula Kiasili” yakikutanisha wadau mbalimbali wa kilimo hai kwa lengo la kuhamasisha kilimo chenye tija na chenye na kutunza mazingira.
