Mtaka Awataka Wakulima Kutoa Taarifa wanapobaini Mbolea zisizokidhi Viwango
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka, amewataka wakulima kutoa taarifa pindi wanapobaini kuwa wamenunua au kukutana na mbolea zisizokidhi viwango, akisisitiza kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kudhibiti pembejeo zisizo na ubora nchini.
Mtaka ameyasema hayo Agosti 13, 2026, alipotembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi 2026 yanayofanyika katika Uwanja wa Dimbani, Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema, ushirikiano baina ya wakulima na Mamlaka ni muhimu katika kukabiliana na wafanyabiashara wanaoingiza na kuuza pembejeo zisizokidhi viwango.
Ameeleza kuwa, mbolea zisizo na ubora zinaweza kuathiri uzalishaji wa mazao na kipato cha wakulima, hivyo ni muhimu kuwa makini wakati wa kununua pembejeo na kutoa taarifa kwa Mamlaka husika wanapobaini bidhaa zinazotia shaka.
“Wakulima wanapaswa kutoa taarifa wanapobaini kuwa wamenunua mbolea zisizokidhi viwango, kwani taarifa hizo zitaisaidia Mamlaka kuchukua hatua na kuwalinda wakulima dhidi ya bidhaa zisizo na ubora,” amesema Mtaka.
Aidha, Mtaka ameitaka TFRA kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa mbolea ya kutosha na yenye ubora katika msimu wa kilimo, ili kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na tija.
Ameongeza kuwa, elimu ya matumizi sahihi ya mbolea imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa mazao katika mikoa mbalimbali nchini, hatua inayosaidia kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima.
