Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
MKUU WA MAGEREZA KILIMANJARO AIPONGEZA TFRA KWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA
06 Aug, 2026
MKUU WA MAGEREZA KILIMANJARO AIPONGEZA TFRA KWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro, SACP Leonard Burushi, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa juhudi zake za kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, akieleza kuwa elimu hiyo ina mchango mkubwa katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

SACP Burushi ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TFRA katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Themi-Njiro, jijini Arusha, ambapo alipata fursa ya kufahamu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Mamlaka katika kusimamia tasnia ya mbolea nchini.

Akitoa maelezo, Meneja wa TFRA Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe, amesema pamoja na kusimamia ubora, usajili, uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa mbolea, Mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji na kulinda afya ya udongo.

Liampawe amesema TFRA imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wakulima katika msimu wa kilimo wa 2026/2027 kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji na ushirikiano na wadau wa sekta ya kilimo, ili kuhakikisha wakulima wanatumia mbolea kwa usahihi na kupata mavuno yenye tija.

Aidha, amesema TFRA itaendelea kutumia maonesho ya Nanenane na majukwaa mengine kuwafikia wakulima kwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya mwaka huu inayohamasisha kuongeza tija ya kilimo kupitia matumizi sahihi ya pembejeo.