Mhe. Mfaume: Tupo Tayari Kuboresha Sheria Kukuza Uwekezaji Tasnia ya Mbolea
Mhe. Mfaume: Tupo Tayari Kuboresha Sheria Kukuza Uwekezaji Tasnia ya Mbolea
Kamati ya Bunge ya Sheria ndogo ndogo chini ya Mwenyekiti wake Mhe.Zuberi Mfaume leo Agosti 4,2026 imefanya Ziara kwenye kiwanda cha kuzalisha mbolea cha Itracom kilichopo eneo Nala jijini Dodoma ili kujionea uzingatiaji wa Sheria, kanuni na miongozo inayosimamia tasnia ya mbolea nchini.
Mwenyekiti Mhe.Zuberi Mfaume na kamati yake wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa namna anavyovutia uwekezaji na kuahidi kumpa ushirikiano mkubwa katika kuendelea kutunga sheria zinazowezesha uwekezaji mkubwa kama uliofanywa na mwekezaji kutoka nchini Burundi.
Amebainisha kuwa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, ipo tayari kupokea mapendekezo ya maboresho ya sheria na kanuni zinazosimamia tasnia ya mbolea pale inapobainika kuwa baadhi ya vifungu vinahitaji kuboreshwa ili kuongeza ufanisi na kuvutia zaidi uwekezaji.
"Nataka niseme tunapoelekea Dira 2050 ambapo sekta binafsi inawezeshwa Kwa asilimia 70 kushiriki katika uchumi wetu, tunahitaji sana mbolea.
Tunahitaji mbolea bora na salama. Hii ni mbolea inayokwenda kuleta uhakika wa uzalishaji, kulinda afya ya udongo wetu na kuongeza tija kwa wakulima," amesema Mhe. Mfaume.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo ameipongeza Mamla ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Kwa Kazi kubwa ya usimamizi wa viwanda vya uzalishaji wa mbolea na maelekezo mazuri wanayoyatoa kwa wazalishaji.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha kuzalisha mbolea cha Introcom Kapten Mstaafu John Chiligati ameishukuru kamati ya Bunge ya Sheria ndogo kwa kuwatembelea na kujiona shughuli zinazofanyika kiwandani hapo.
Amesema mbolea inayozalishwa kiwandani hapo ni mbolea bora si Afrika tu bali ulimwenguni kote.
