Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
DC TABORA: ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA NA AFYA YA UDONGO IPEWE KIPAUMBELE
05 Aug, 2026
DC TABORA: ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA NA AFYA YA UDONGO IPEWE KIPAUMBELE

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na umuhimu wa kupima afya ya udongo ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao.

DC Wella ametoa rai hiyo alipotembelea banda la TFRA katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Ipuli, mkoani Tabora, ambapo amepongeza juhudi za Mamlaka katika kuwafikia wakulima kwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TFRA Kanda ya Kati, Allan Mariki, amesema Mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea kwa kuzingatia mahitaji ya mazao na matokeo ya upimaji wa afya ya udongo ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya mbolea.

Mariki amesema katika msimu wa kilimo wa 2026/2027, TFRA itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wengi zaidi wanapata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kupitia vipindi mbalimbali vinavyotarajiwa kuanza kurushwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Channel ten.