Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
WATANZANIA WAMETAMBUA FURSA ZILIZOPO TASNIA YA MBOLEA
11 Jul, 2025
WATANZANIA WAMETAMBUA FURSA ZILIZOPO  TASNIA YA MBOLEA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema, kwa sasa watanzania wametambua umuhimu wa mbolea katika kuongeza tija ya kilimo na kuibua fursa za kiuchumi kwenye mnyororo wa thamani wa tasnia ya mbolea. 

Laurent ametoa kauli hiyo tarehe 10 Julai, 2025 akizungumza na waandishi wa habari ndani ya banda la Mamlaka katika viwanja vya Mwl. J.K Nyerere yanakoendelea maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara.

Akifafanua kauli hiyo, Mkurugenzi Joel amesema mnamo mwaka 2021/2022   matumizi ya mbolea nchini yalikuwa ni tani 363,599 na kufikia Juni 2024/2025 matumizi yaliongezeka na kufikia tani 848,884 huku tukitarajia matumizi hayo kuongezeka zaidi ya tani 1,000,000 kwa mwaka.

Laurent ameeleza kuwa, ongezeko la matumizi ya mbolea linaenda sambamba na jitihada mbalimbali za Serikali na wadau za kuhakikisha wakulima wanapata mbolea sahihi kwa wakati sahihi, kulingana na mahitaji halisi ya udongo. 

Akizungumzia fursa za kibiashara zilizoko kwenye tasnia ya mbolea Laurent  amesema, kufuatia utekelezaji wa mpango wa ruzuku uhitaji wa pembejeo hiyo umekuwa mkubwa na kuibua wafanyabiashara wengi wanaonufaika na biashara hiyo ambayo  gharama ya usafirishaji imeunganishwa kwenye bei ya mbolea na hivyo kuwafanya wafanyabiashara kupata faida wanayoitarajia.

“Mwaka 2022, Watanzania wengi hawakuweza kuona fursa zilizopo kwenye sekta ya mbolea kutokana na matumizi hafifu, lakini leo tunaiona Tanzania ikielekea kuwa fertilizer hub ya Afrika,” anasema Mkurugenzi Laurent.

 “Tunatarajia ifikapo mwaka 2030, Tanzania itakuwa na mahitaji makubwa zaidi ya mbolea kutokana na kuongezeka kwa matumizi na mabadiliko ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo biashara,” Laurent ameongeza. 

Pia, Laurent amesema, kufuatia kuimarika kwa miundombinu ya bandari, upanuzi wa viwanda vya ndani na jitihada za Serikali katika kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, miaka mitano ijayo Tanzania itaibuka na kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa mbolea barani Afrika. 

Amesema, katika kukuza biashara ya mbolea, TFRA inasimamia mfumo maalum wa usajili na usambazaji wa mbolea kwa njia ya kidijitali. Mfumo huu unasaidia pia katika usambazaji wa mbegu za ruzuku, ambapo wakulima wanatakiwa kujisajili ili kunufaika. 

“Nasisitiza kwa Watanzania kuendelea kujisajili na kuhuisha taarifa zao katika mfumo huu ili kuendelea kunufaika na ruzuku na huduma nyingine muhimu,” anasema mwakilishi wa TFRA.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa watembeaji katika banda la Mamlaka kwa Mkurugenzi Mtendaji Laurent, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi, Azizi Mtambo amesema toka maonesho yaanze wamepokea watembeaji 564.

Amesema, miongoni mwa watembeaji hao, 59 waliomba leseni ya biashara ya mbolea na watembeaji 102 wamejisajili na kuhuisha taarifa zao kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku.