WAKULIMA KANDA YA MASHARIKI WANUFAIKA HUDUMA USAJILI PEMBEJEO ZA RUZUKU.
Mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania TFRA imesogeza huduma ya usajili wa wakulima katika mfumo wa pembejeo za ruzuku kwenye maonesho ya wakulima wafugaji na wavuvi nanenane.
Katika kanda ya Mashariki viwanja vya Mwl. Julius Nyerere huduma ya usajili wa wakulima imeshika kasi na kufurahiwa na watembeleaji wengi.
Akielezea utoaji wa huduma hiyo afisa udhibiti ubora mwandamizi TFRA kanda ya Mashariki Raymond Konga amesema wakulima wanahamasika kujisajili kwenye mfumo baada ya kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Konga ameongeza kuwa ongezeko la usajili wa wakulima kwenye mfumo linatafsiri ongezeko la matumizi ya mbolea katika msimu ujao wa kilimo na kuongeza uhakika wa mavuno.
Katika maonesho hayo wakulima, wafanyabiashara wa mbolea na wadau wengine wa mbolea hupatiwa huduma mbalimbali ikiwemo kujibiwa maswali papo hapo, usajili wa wakulima na utoaji wa leseni za biashara ya mbolea.
