Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Waingizaji/wasambazaji wa mbolea nchini waaswa kuwekeza kwenye uzalishaji
07 Aug, 2025
Waingizaji/wasambazaji wa mbolea nchini waaswa kuwekeza kwenye uzalishaji

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ametoa wito kwa kampuni za uingizaji na usambazaji wa mbolea nchini kuhakikisha zinajielekeza zaidi kwenye uwekezaji wa uzalishaji wa ndani ili kusaidia upatikanaji endelevu wa mbolea kwa wakulima kwa gharama nafuu.

"Serikali inatamani kuona sekta binafsi ikiendelea si tu kama wasambazaji wa mbolea, bali kama washirika wa maendeleo wanaowekeza katika uzalishaji wa ndani wa mbolea, ili kusaidia kupunguza gharama kwa wakulima na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati," amesema Joel Laurent.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 6 Agosti 2025, wakati wa ziara yake kwa wadau wa mbolea kwenye Kijiji cha Mbolea katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Laurent amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa mbolea nchini, huku akitoa pongezi kwa kampuni alizozitembelea  kwa juhudi zao za kufikisha mbolea kwa wakulima na kuwekeza katika elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.

Ameongeza kuwa ni dhamira ya Serikali kupitia Agenda 10/30: Kilimo ni Biashara kuhakikisha kuwa taifa linajitosheleza kwa pembejeo hiyo kwa kutumia uzalishaji wa ndani.

Pia amezihimiza kampuni kutumia maonesho haya kutoa taarifa ya upatikanaji wa mbolea zao kwa wakulima pamoja na kushirikiana na TFRA katika utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima.

Ikiwa ni siku ya pili ya ziara katika banda la Kijiji cha Mbolea, Mkurugenzi Joel ametembelea kampuni za ETG Inputs Limited, YARA Tanzania Limited, Crop Guard, MeTL GROUP, Paramount Commodities LTD, Mwana wa Afrika, BioGrow, PREMIUM AGRO CHEM LTD, OCP na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya kuboresha tasnia ya mbolea nchini.