Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Serikali yafikia asilimia 83 ya lengo la upatikanaji wa mbolea nchini
28 Apr, 2026
Serikali yafikia asilimia 83 ya lengo la upatikanaji wa mbolea nchini

Waziri wa Kilimo, Mhe.Daniel Chongolo, amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania imefanikiwa kuratibu upatikanaji wa tani milioni  1,254,203 za mbolea hadi kufikia mwezi Machi 2026, ikiwa ni asilimia 83.61 ya lengo la tani 1,500,000 kwa msimu wa kilimo 2025/2026.

Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma, Aprili 28, 2026, Mhe. Chongolo   amesema kati ya kiasi hicho, tani 150,686 zimezalishwa ndani ya nchi, tani 869,840 zimeagizwa kutoka nje na tani 233,677 ni bakaa iliyokuwepo nchini kutoka msimu uliopita wa kilimo.

Mhe. Chongolo amebainisha kuwa, kwa mwaka 2026/2027, Wizara kupitia TFRA imepanga kuratibu upatikanaji wa tani milioni 1.5 za mbolea na kuzisambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku.

Aidha, Mhe.Chongolo amesema Tani 674,686.24 za mbolea zimesambazwa kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku katika mikoa yote na usambazaji unaendelea. 

Amesema, hatua hiyo imeongeza kiwango cha matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 za virutubisho mwaka 2021/2022 hadi kufikia wastani wa kilo 27 za virutubisho kwa hekta mwaka 2025/2026 ambayo ni sawa na asilimia 54 ya lengo la kilo 50 za virutubisho kwa hekta kulingana na azimio la CAADP.