Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TADCOS kufanya kazi na Serikali
29 May, 2024
TADCOS kufanya kazi na Serikali

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amewatoa hofu wawakilishi wa Jumuiya ya Mawakala wa Pembejeo nchini (TADCOS) na kueleza Serikali inathamini mchango wao katika usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima nchini.



"kufuatia wasilisho mlilolitoa nimeona kitu kikubwa sana kitakachosaidia kuongeza tija kwenye usambazaji wa pembejeo kwa wakulima nchini" Naibu Waziri Mavunde aliongeza.



Naibu waziri Mavunde amesema hayo leo mara baada ya kupokea wasilisho kutoka kwa Mwasilishaji kutoka jumuiya hiyo wakiitaka serikali kuwatumia katika usambazaji wa pembejeo kwa wakulima na si kuweka nguvu zaidi kwa makampuni makubwa ya uingizaji wa mbolea.



Mavunde ameongeza kuwa, Wizara inaichukulia jumuiya hiyo kama mdau muhimu sana katika Sekta ya Kilimo na kueleza hakuna namna Serikali itakwenda kinyume nao na kuthamini kampuni kubwa pekee za pembejeo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gelard Mweli akiongea na wawakilishi wa Jumuiya ya Mawakala wa Pembejeo nchini (TADCOS)

Kuhusu changamoto wanazozipata kupitia mfumo wa mbolea za ruzuku, Mavunde ameeleza kuwa mfumo huo ni mpya na maboresho yanaendelea kadri changamoto zinavyoibuliwa.



"Changamoto mlizokutana nazo mwezi Septemba, 2022 ni tofauti na mnazokutana nazo kutokana na ukweli kwamba changamoto zinasikilizwa na kutatuliwa kila mara" Mavunde alisisitiza.



Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gelard Mweli, amesema wizara yake itafanya kazi na wafanya biashara wakubwa na mawakala wa pembejeo wakubwa kwa wadogo na hivyo kuwapunguzia changamoto wakulima.



Aidha, Katibu Mkuu Mweli amewahakikishia Mawakala hao kuwa wao ndio wanaojua vyema namna biashara inavyofanyika na kueleza wizara ni wawezeshaji tu.



Amesema, moja kati ya changamoto kubwa ya wakulima ni ucheleweshwaji wa pembejeo na kubainisha ili kufikia Agenda 10:30 Kilimo ni Biashara kuna umuhimu wa kuboresha mfumo wa pembejeo.



"Sasa tunatamani ifikapo Mwezi Julai, mkulima anapokwenda kuuza mazao yake akutane na pembejeo katika maghala anunue na kuhifadhi kwa ajili ya msimu unaofuata wa kilimo" Alisisitiza Mweli.



Mmekuja na wasilisho lenye mantiki kubwa katika kutatua changamoto za wakulima", Mweli alikazia.



Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ushirika wa Mawakala TADCOS Gerlad Filbert alisema lengo la kuanzishwa kwa ushirika huo ni kuwasaidia wakulima kwa kuwafikishia pembejeo kwa umbali usiozidi Kilomita 3 (tatu) kutoka wanakofanyia shughuli zao za kilimo.



Pamoja na manufaa mengine ya uwepo wa ushirika huo Filbert amesema TADCOS itaiwezesha Serikali kuwasimamia mawakala kwa urahisi pamoja na kusaidia kuondoa pembejeo bandia sokoni.