Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Serikali Yatoa Elimu ya matumizi sahihi na Uchanganyaji Mbolea za Kupandia
16 Oct, 2025
Serikali Yatoa Elimu ya matumizi sahihi na  Uchanganyaji Mbolea za Kupandia

Wakulima wa vijiji vya Ujindile, Wangama, Kipengere na Mwilamba vilivyopo halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe Mkoani Njombe wameishukuru serikali kwa kuwapa elimu iliyowajengea uwezo wa matumizi sahihi ya mbolea sambamba na namna bora ya kuchanganya mbolea tofauti tofauti ili kupata mbolea kwa ajili ya kupandia mazao.

Wamefundishwa kuwa, ukichanganya mifuko miwili ya mbolea ya TSP yenye kirutubisho chenye asilimia 46 ya Fosiforasi na mfuko mmoja wa mbolea ya CAN wenye Nitrojeni asilimia 27 unakuwa umepata mifuko mitatu kwa ajili ya mbolea ya kupandia yenye sifa nzuri zaidi ya mbolea ya DAP huku ukiwa umeokoa  gharama ya kununua pembejeo hiyo.

Wakiongea baada ya kupatiwa elimu katika mikutano ya hadhara ambayo imefanyika katika vijiji vinne wilayani Wanging'ombe wakiwemo Abedinego Nsemwa na Wende Adamsom wamesema kitendo cha kupatiwa ujuzi huo kimewafungua macho na kwamba wanategemea kwenda kuongeza uzalishaji wa viazi, mahindi na mazao mengine yanayotumia mbolea za chumvichumvi huku wengine wakisema kuanzia sasa hawaoni changamoto tena ya mbolea za kupandia.

Awali Samwel Msongwe Afisa Masoko kutoka kampuni ya mbolea nchini (TFC) pamoja na Joshua Joel ambae ni mtaalamu wa kilimo kutoka kampuni binafsi wakifundisha kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo hususani mbolea wamesema mkulima anapaswa kutambua kila mbolea ina wakati wake sahihi wa kutumika hivyo endapo makosa yatafanyika athari zitajitokeza kwenye mavuno.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent ameeleza kusudio la serikali kuendesha zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa sekta ya kilimo na kisha kutoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaoihujumu serikali kwa kuuza mbolea nje ya mfumo wa ruzuku.