RC Songwe Awataka Wakulima Kutumia Mbolea kwa Kuzingatia Afya ya Udongo – Nane Nane 2025

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabiri Omari Makame, amewataka wakulima kote nchini kuhakikisha wanatumia mbolea kwa kuzingatia afya ya udongo badala ya kufanya matumizi kwa mazoea au kubahatisha huku akisisitiza kuwa matumizi sahihi ya mbolea ni msingi wa kuongeza tija katika kilimo na kulinda ardhi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
“Tunahitaji matumizi ya mbolea yaendane na afya ya udongo. Hili ni jukumu la kila mkulima, na serikali imehakikisha vifaa vya kupimia udongo vinapatikana kila halmashauri. Tuchukue hatua, tusibahatishe,” alisema Mheshimiwa Makame.
Kauli hiyo ameitoa tarehe 3 Agosti 2025 wakati wa ziara yake katika banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale, mkoani Mbeya, ambapo alikuwa mgeni wa siku.
Katika maelekezo yake kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa vifaa vya kupima afya ya udongo tayari vinapatikana katika kila halmashauri nchini, hivyo hakuna sababu ya kutotumia taarifa sahihi za udongo kabla ya kutumia mbolea. Ametoa wito kwa wakulima kuwa na tabia ya kufuatilia hali ya udongo wao mara kwa mara.
Pamoja na agizo hilo, Mheshimiwa Makame ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na utoroshaji wa mbolea nje ya nchi au uchakachuaji wa pembejeo hizo muhimu, akisema vitendo hivyo vinahujumu juhudi za serikali katika kuendeleza kilimo.
“Hatutasita kuchukua hatua kali kwa wale wanaotorosha mbolea au kuchakachua. Tumejipanga kuhakikisha kila mfuko wa mbolea unaowasili kwa mkulima ni salama, sahihi, na una mchango chanya kwa uzalishaji,” Mhe. Makame amesisitiza.
Pia Mhe. Makame amebainisha kuwa, serikali kwa kushirikiana na taasisi kama TFRA imejipanga kuleta mapinduzi ya kweli katika sekta ya kilimo kupitia usimamizi madhubuti wa pembejeo, elimu kwa wakulima na udhibiti wa ubora wa mbolea na pembejeo zinginezo za kilimo ili kuongeza tija na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Maonesho ya Nane Nane ya mwaka huu yanafanyika katika kanda 6 yakiwa na kauli mbiu inayosema “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”.