Rais Samia: Matumizi sahihi ya Mbolea Kuinua Sekta ya Kilimo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema maendeleo ya kweli Barani Afrika hayawezi kufikiwa bila kuimarishwa kwa sekta ya kilimo, huku akisisitiza kuwa sekta hiyo haiwezi kustawi bila matumizi sahihi ya mbolea.
Mhe. Rais ameyasema hayo leo jijini Dodoma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea cha Itracom kilichopo eneo la Nala.
Akihutubia katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Mej. Jenerali Evariste Ndayishimiye , pamoja na wawekezaji na viongozi mbalimbali wa serikali Rais Samia amesema Serikali imedhamiria kumwinua mkulima kwa kuweka msukumo kwenye maeneo ya kipaumbele ikiwemo kuongeza bajeti ya kilimo ili, kuimarisha huduma za ugani na kupima afya ya udongo.
"Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi duniani. Nawaambia wazi kuwa mmewekeza kwenye sekta muhimu sana, na hakika itawalipa zaidi ya mlichowekeza," amesisitiza Rais Samia.
Aidha, Mhe. Rais ametoa wito kwa wawekezaji wa kiwanda hicho kuhakikisha mbolea inayozalishwa inauzwa kwa bei nafuu na himilivu, ili wakulima waweze kuimudu na kutumia kwenye uzalishaji kwa tija, hasa ikizingatiwa kuwa malighafi nyingi za mbolea hiyo zinapatikana hapa nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo Rais wa Burundi Mhe.Evarist Ndayishimiye, ameonesha kufurahishwa kwa kuwa miongoni wa mashuhuda wa uzinduzi rasmi wa kiwanda hicho ambacho mnamo tarehe 22 Oktoba, 2021 walikutana na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wake.
Ameeleza kuwa, Kiwanda cha mbolea cha Itracom ni kampuni tanzu ya FOMI Fertilizers ambayo makao yake makuu yapo nchini Burundi ambayo pia inazalisha na kusambaza mbolea kama hizi kwa wakulima wa Burundi.
"Hii ni ishara nzuri ya ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Burundi" Rais .
Ndayishimiye alisisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amesema kuwa katika sera za maendeleo ya nchi, kilimo kinapewa nafasi ya kwanza. "Tumejikita kwenye maeneo manne makuu: kuboresha afya ya udongo, kuongeza matumizi ya mbolea, kuimarisha umwagiliaji na kutumia teknolojia ya kisasa (mechanization)," amesema Prof. Mkumbo.
Ameeleza kuwa, hatua ya kuzindua kiwanda hicho ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais kuhusu kuvutia uwekezaji kwenye maeneo ya uzalishaji, hususan sekta ya kilimo na viwanda.
Naye Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohamed Bashe, amesema kuwa matumizi ya mbolea nchini yameongezeka maradufu kutokana na juhudi za serikali kutoa ruzuku. "Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, na matumizi yamepanda kutoka tani 360,000 mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 840,000 mwaka 2024/2025," amesema Mhe. Bashe.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msukumo mkubwa katika kupeleka maendeleo vijijini kwa kuimarisha huduma za maji, barabara, na umeme—huku yote haya yakiwa ni jitihada za kuwagusa wakulima na kuchochea maendeleo ya kilimo nchini.