Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Mkuu wa Mkoa Morogoro aipongeza TFRA kwa Usimamizi mahiri Tasnia ya Mbolea
04 Aug, 2025
Mkuu wa Mkoa Morogoro aipongeza TFRA kwa  Usimamizi mahiri Tasnia ya Mbolea

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kazi nzuri ya kusimamia na kudhibiti ubora wa mbolea nchini, akibainisha kuwa Mamlaka hiyo imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Pongezi hizo amezitoa tarehe 4 Agosti 2025, alipofanya ziara katika banda la TFRA kwenye Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya J.K. Nyerere, mkoani Morogoro.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Malima alisema kuwa kwa sasa wakulima wengi wanatumia mbolea kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Mamlaka hiyo katika kutoa elimu na kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya. Hii ni kazi kubwa na yenye manufaa kwa wakulima wetu. Mmeanza safari kutoka mbali, na mafanikio yenu yanaonekana wazi. Kuna mabadiliko makubwa sana katika sekta hii,” alisema Mhe. Malima.

Aidha, aliihimiza TFRA kuendelea kuongeza jitihada katika kuwaelimisha na kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea kwa wingi ili kuongeza tija kwenye kilimo na kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja pamoja na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Aziz Mtambo, amemueleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa inatekeleza  majukumu mbalimbali yakiwemo ya usimamizi wa mpango wa mbolea ya ruzuku pamoja na kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea katika Mkoa wa Morogoro na maeneo mengine nchini.

Katika banda hilo, Mhe. Malima amepokelewa na Mjumbe wa Bodi ya TFRA, Dkt. Catherine Senkoro, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Anthony Diallo na menejimenti ya Mamlaka.

Maonesho haya ya Nane Nane ni fursa muhimu kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kujifunza, kupata elimu sahihi kuhusu matumizi ya mbolea, pamoja na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na TFRA katika kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora, salama na yenye viwango stahiki.