Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
MAONESHO YA PARACHICHI KUIMARISHA KILIMO CHA KISASA NA TIJA KWA WAKULIMA BUSOKELO
12 Oct, 2026
MAONESHO YA PARACHICHI KUIMARISHA KILIMO CHA KISASA NA TIJA KWA WAKULIMA BUSOKELO

Wakulima wa zao la parachichi wametakiwa kutumia fursa za maonesho ya parachichi yanayofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya kujifunza mbinu za kisasa za kilimo zitakazoongeza uzalishaji na tija pamoja na kuboresha kipato chao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya.

Akizungumza katika ufunguzi wa maonesho hayo, Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Thadei Ngambila aliyemwakilisha Katibu Tawala Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Mbeya amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa wakulima kupata elimu na teknolojia za kisasa zitakazowasaidia kuzalisha parachichi bora na kuongeza thamani ya zao hilo.

Ngambila amewataka wataalamu wa kilimo kutumia fursa hiyo kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima kuhusu uzalishaji wa parachichi, akisisitiza kuwa mkulima anapofanya shughuli zake bila kushirikiana na wadau wengine katika mnyororo wa thamani anaweza kukosa fursa muhimu za kuongeza tija na kunufaika kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Afisa Udhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mushoborozi Christian ameeleza kuwa maonesho hayo yatawasaidia wakulima kufahamu faida na umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa parachichi, ikiwemo kuboresha afya ya udongo na kuongeza ubora wa mazao. Amehimiza wakulima kupata ushauri kutoka kwa wataalamu ili waweze kuchagua na kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na zao husika.

Kwa upande wake, mkulima wa zao la parachichi Prisca Butuyuyu amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo, akisema kuwa yana nafasi kubwa ya kuongeza uelewa na mwamko kwa wakulima kujikita katika uzalishaji wa parachichi wenye tija, huku akibainisha umuhimu wa kuendelea kuandaa majukwaa yatakayowaunganisha wakulima na wadau mbalimbali wa zao hilo.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza uelewa kuhusu afya ya udongo na matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kukuza ushirikiano kati ya wakulima na wadau wengine ili kuongeza uzalishaji na manufaa ya zao la parachichi kwa wakulima na uchumi wa eneo hilo.