MAKAME AITAKA TFRA KUHAKIKISHA WAKULIMA WA SONGWE WANAPATA MBOLEA KWA WAKATI NA BEI YA RUZUKU
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabiri Omari Makame, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha wakulima wa mkoa huo wanapata mbolea ya kutosha kwa wakati na kwa bei ya ruzuku, kufuatia malalamiko ya baadhi ya wakulima kuhusu kuuziwa mbolea kwa bei isiyo rasmi.
Mhe. Makame ametoa maelekezo hayo leo Agosti 2, 2026 alipotembelea banda la TFRA katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt John Mwakangale mkoani Mbeya, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa biashara ya mbolea ili wakulima wanufaike na ruzuku inayotolewa na Serikali.
Akitoa ufafanuzi, Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’odya, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa hakuna upungufu wa mbolea nchini na kwamba TFRA inaendelea kufuatilia upatikanaji na usambazaji wake ili kuwafikia wakulima kwa wakati.
Ng’odya amesema kwa sasa nchini kuna tani 248,617 za mbolea za aina mbalimbali zilizopo kwenye maghala ya wazalishaji, waagizaji na wasambazaji, huku Mkoa wa Songwe ukiwa na tani 11,494.06 ambazo zinaendelea kuuzwa kwa wakulima.
Amesema kupanda kwa bei ya mbolea katika kipindi cha hivi karibuni kumechangiwa na athari za mabadiliko katika soko la dunia yaliyotokana na mgogoro wa kimataifa kati ya Iran na Marekani, hata hivyo Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya pembejeo ili kupunguza gharama kwa wakulima na kuhakikisha wanapata mbolea kwa bei nafuu.
Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mbolea nchini, ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwekezaji katika viwanda vya mbolea, ili kufikia mwaka 2030 Tanzania ipunguze utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi na kujitosheleza kwa uzalishaji wa ndani.
Amesisitiza kuwa TFRA itaendelea kufuatilia kwa karibu upatikanaji, usambazaji na uuzaji wa mbolea nchini ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo hiyo muhimu kwa wakati na kwa bei stahiki, sambamba na kulinda maslahi yao.
