Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Dola Milioni 2 za Kimarekani Kununufaisha Wakulima nchini
08 Aug, 2025
Dola Milioni 2 za Kimarekani Kununufaisha Wakulima nchini

Wakulima wadogo zaidi ya 550,000 nchini Tanzania watanufaika na upatikanaji wa mbolea kupitia mradi mpya wa Dhamana ya Mikopo ya Biashara kwa Sehemu (Partial Trade Credit Guarantee – PCG), baada ya dola milioni 2 za Kimarekani kutengwa kwa ajili ya kuwawezesha wauzaji wa pembejeo kupata mbolea kwa mkopo.

Upatikanaji wa kiasi hicho cha fedha utawawezesha wauzaji wadogo wa pembejeo za kilimo kufikisha pembejeo hizo kwa wakulima kwa wakati.

Mradi huo umezinduliwa rasmi tarehe 7 Agosti, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao, Usalama wa Chakula na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi, katika viwanja vya Maonesho ya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.

Akizindua mradi huo, Dkt. Nindi, amesema kuwa, serikali imejidhatiti kuhakikisha wakulima walioko pembezoni wanawezeshwa kwa kupata pembejeo bora kupitia mifumo rafiki ya kifedha inayohusisha sekta binafsi.

Amesema, mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Mfuko wa Ufadhili wa Mbolea Afrika (AFFM), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), na mshirika mtekelezaji African Fertilizer and Agribusiness Partnership (AFAP), kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mbolea bora na kwa wakati kwa wakulima wadogo nchini.

“Mradi huu utatekelezwa kupitia sekta binafsi ambapo mawakala wa mbolea watawezeshwa kupata mbolea kwa mkopo, huku wakitoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima,” alisema Dkt. Nindi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema, mradi huo ni mwendelezo wa mafanikio yaliyopatikana kati ya mwaka 2019 hadi 2022 katika awamu ya awali ya utoaji wa dhamana za mikopo ya mbolea. Amesisitiza kuwa awamu hii inalenga zaidi kuwezesha wakulima wadogo kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

“Awamu hii inalenga si tu kupunguza hatari katika sekta ya kilimo, bali pia kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi, na muhimu zaidi kuwawezesha wakulima wadogo ambao ndio uti wa mgongo wa uzalishaji wa chakula nchini,” amesema Joel.

Akizungumza kwa muktadha mpana wa bara la Afrika, Joel ameongeza kuwa, uzinduzi wa mradi huu unaendana na azma ya kisera ya bara hilo, hasa baada ya Mkutano wa Mbolea na Afya ya Udongo uliofanyika Mei 2024 jijini Nairobi, ambapo Tamko la Nairobi lilipitishwa likilenga kuongeza mara tatu upatikanaji wa mbolea bora barani Afrika ndani ya miaka 10.

Mradi huu wa PCG, kwa mujibu wa TFRA, ni sehemu ya mchango wa Tanzania katika mageuzi hayo ya kilimo barani Afrika, hasa kwa kushughulikia changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha na upatikanaji mdogo wa pembejeo kwa wakulima wadogo.

Akihitimisha, Joel ameushukuru Mfuko wa Ufadhili wa Mbolea Afrika (AFFM) kwa ushirikiano na kujitolea kwao katika kuimarisha upatikanaji wa mbolea, sambamba na kushiriki kikamilifu katika maonesho ya mwaka huu kwa kuweka banda mahsusi ndani ya Kijiji cha Mbolea, ili kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu miradi inayoendelea kutekelezwa.

Naye Marie Claire Kalihangabo, Mratibu wa Mradi kutoka AFFM, amesema cha dola milioni 2 za kimarekani kimetengwa kama dhamana itakayowasaidia wauzaji wa kati na wadogo kupata mbolea kwa mkopo kutoka kwa wasambazaji wakubwa, huku AFFM wakigawana hatari (risk) ya kifedha itakayotokana na mikopo hiyo na wasambazaji kwa usawa.

Aidha, Kalihangabo amesema mradi huo unatarajiwa kuhusisha wasambazaji wakubwa watatu (3), wauzaji wa kati wapatao 30, na zaidi ya wauzaji wa rejareja 1,000, huku ukitarajiwa kuwanufaisha wakulima kwa kuwafikishia takribani tani 60,000 za mbolea katika kipindi cha miezi 36 ijayo.

Amehitimisha kwa kusema, AFAP, kama mshirika mtekelezaji, itapata msaada wa dola 528,600 za Kimarekani kwa ajili ya utekelezaji na usimamizi wa mradi.