Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
MAONESHO YA KILIMO AFRIKA: WAWEKEZAJI WA MBOLEA 20 WAJITOKEZA
04 Sep, 2026
MAONESHO YA KILIMO AFRIKA:  WAWEKEZAJI  WA MBOLEA  20  WAJITOKEZA

Zaidi ya kampuni 20 zimeonesha nia ya kuwekeza katika tasnia ya mbolea nchini Tanzania, kufuatia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizoainishwa wakati wa Maonesho ya Kumi ya Kilimo yanayofanyika kwa siku mbili katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Akizungumza leo, Septemba 2, 2026, Meneja Sehemu ya Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Getrude Ng’weshemi, amesema kampuni hizo zimeonesha kuvutiwa na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa tasnia ya mbolea nchini hususani mbolea hai.

Ng’weshemi amesema baadhi ya kampuni zimeonesha nia ya kuwekeza katika eneo la ujenzi wa viwanda vya kuzalisha, uchanganyaji na uingizaji wa mbolea, zikiwemo mbolea za asili na za viwandani.

“Maonesho haya yametupa fursa kubwa ya kuwafikia wawekezaji na kuwaeleza fursa zilizopo katika tasnia ya mbolea. Tumeshuhudia kampuni zaidi ya 20 zikionesha nia ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya tasnia hii kutoka mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na India na Misri,” amesema Ng’weshemi.

Kwa upande wake, Meneja wa Sehemu ya Usajili na Leseni wa TFRA, Mwahija Irika, amesema Mamlaka hiyo imepata fursa ya kushiriki katika mkutano uliofanyika sambamba na maonesho hayo, ambapo iliwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika tasnia ya mbolea nchini.

Irika amesema miongoni mwa fursa hizo ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha na kuchanganya mbolea, uzalishaji wa vifungashio vya mbolea pamoja na uwekezaji katika uwakala na usambazaji wa mbolea.

Amesema uwekezaji katika maeneo hayo ni muhimu katika kuhakikisha mbolea inapatikana kwa wakati na kwa urahisi zaidi, hasa kwa wakulima walioko katika maeneo ya pembezoni nchini.

Maonesho hayo ya Kilimo yanatoa fursa kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya kilimo, wakiwemo wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za Serikali, kuonesha bidhaa, huduma na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta hiyo.