WEKEZENI KATIKA TAFITI ZA MBOLEA BORA – PROF. MKENDA

Serikali imewaagiza wataalamu wa kilimo kutoka katika taasisi mbalimbali za Utafiti kuwekeza na kutafiti aina bora za mbolea na kutoa utaalamu huo kwa viwanda vya mbolea nchini ikiwemo kiwanda cha mbolea cha Minjingu hatua ambayo itasaidia nchi kuacha kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda wakati wa ziara yake Mkoani Manyara alipotembelea kiwanda cha Mbolea cha Minjingu hivi karibuni ambapo aliongozana na wataalamu kutoka katika taasisi za utafiti ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA), Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT), Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI)naTaasisi ya Utafiti wa KilimoTanzania (TARI).
Prof. Mkenda alisema ni wajibu wa wataalamu wa utafiti wa kilimo katika mazao mbalimbali kufanya utafiti utakaosaidia kugundua mbolea bora na zenye matokeo mazuri kwa wakulima, jambo ambalo litapunguza gharama za uingizwaji wa mbolea kutoka nje ya nchi.
“Nawaagiza wataalamu kutoka katika taasisi za kilimo kufanya utafiti utakaosaidia kiwanda cha Minjingu kuzalisha mbolea zitakazofanya vizuri kama ambazo tumekuwa tukiagiza Nje ya Nchi, njia ya kuzalisha mbolea hizo mnazo na sio siri”. Alisema Prof. Mkenda.
Alisema Tanzania imekuwa ikitumia zaidi ya dola milioni 200 kuagiza mbolea kutoka nje kila mwaka kwa kutumia fedha za wakulima na kwamba iwapo bidhaa hiyo itazalishwa nchini italeta tija zaidi kwa taifa tofauti na ilivyo sasa.
“Kimsingi tunatumia pesa za wakulima ni hasara….kile ambacho kinaweza kuzalishwa hapa ambacho hakiwezi kutuongezea bei kizalishwe hapa mambo ya pembejeo tukiendelea kuagiza hatutasonga mbele” alisema Waziri Mkenda.
“Watafiti wasaidieni hawa wazalishaji wetu wa ndani kutengeneza bidhaa zanye ubora na mnafahamu Minjingu wanaweza kufanya, tumsaidie afanye hivyo maana watu wetu watapata ajira, TRA watakusanya mapato zaidi na taifa kupata mapato mengi zaidi” alisema.
Prof. Mkenda aliongeza kuwa serikali katika mwaka huu wa fedha (2021/2022) itaongeza fedha katika sekta ya kilimo eneo la utafiti na ugani hatua ambayo itasaidia kukipeleka kilimo katika maendeleo ya uchumi shindani.
Amesema sambamba na mpango wa miaka mitano wa kuboresha sekta ya kilimo wananchi wanahitaji mazao ya chakula yashuke bei lakini mkulima naye apate fedha na faida kwani hii inawezekana kwa wakulima kulima kilimo chenye tija eneo dogo kwa mazao mengi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Minjingu, Tosky Hans, alisema kiwanda hicho kimejiwekea mkakati wa kuongeza uzalishaji kutoka tani laki moja hadi kufikia tani laki tano ifikapo mwaka 2025 kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko la ndani.
“Tunafahamu serikali imeweka malengo la kukuza sekta ya kilimo tumeanza kuzungumza na Taasisi za kifedha kwa ajili ya kutukopesha na kupanua kiwanda chetu, kiwanda kinatengeneza mbolea za aina tofauti tofauti kulingana na mazao na mbolea hizi zimesheheni aina mbalimbali za virutubisho vya udongo” Aisema Bw. Hans.
Aidha alisema kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya Serikali kutolipa malimbikizo ya deni la mbolea za ruzuku la mwaka 2015/2016 na kulipishwa kodi za VAT kuingiza mali ghafi.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Joseph Mkirikiti, alisema baadhi ya maafisa ugani wamekuwa hawaendi mashambani kwa wakulima na kubaki maofisini jambo ambalo wanapaswa kubadilika kwa lengo la kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo.
Akizungumza mapema, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Bi. Veronica Sophu anayewakilisha wakulima wadogo kupitia MVIWATA, ameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuvikopesha vyama vya ushirika vya wakulima ili waweze kununua mbolea kwa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS), hatua itakayosaidia wakulima kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.
Mjumbe huyo ambaye pia ni mkulima wa mpunga toka Madibira wilaya ya Mbarali alibainisha kuwa wanachama wake wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa njia ya umwagiliaji na matumizi ya mbegu na mbolea bora ambayo imeongeza uzalishaji kutoka gunia 25 kwa hekta hadi kufikia tani 7 hadi 10 mwaka 2019.
“Vyama vya ushirika vikitumika kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja itasaidia wakulima kufikishiwa bidhaa hiyo kwa bei nafuu huku ikiwa imezingatia aina ya zao wanalozalisha” alisema Bi. Sophu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA Prof. Anthony Mshandete ameipongeza serikali kwa maelekezo ambayo imekuwa ikiyatoa hatua inayosaidia Bodi yake kuwafikia wakulima wengi kwa kufikisha mbolea inayohitajika kupitia BPS.
“Mkakati wetu ni kuhamasisha watanzania wengi waanzishe viwanda vya mbolea hapa nchini hali itakayosaidia kupata mbolea bora na yenye gharama nafuu hivyo kuachana na utegemezi wa mbolea toka nje ya nchi” alihitimisha Prof. Mshandete.