MBOLEA YA RUZUKU YAONGEZA UZALISHAJI ILEJE

Halmashauri ya Wilaya ya Ileje imepiga hatua kubwa katika matumizi ya mbolea kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji, hatua inayochochewa na msisitizo wa Serikali wa kuhakikisha uzalishaji wenye manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla kupitia kampeni ya “Mali Shambani: Silaha Mbolea.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Nuru Waziri Kindamba, amesema wananchi wa Ileje wamekuwa mstari wa mbele kutumia mbolea ili kuongeza mavuno, jambo lililosaidia kuimarisha uchumi wa kaya na kuchochea maendeleo.
“Tumeweza kutumia tani 6,460 za mbolea kwa msimu wa 2024/2025, hatua iliyosaidia kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 60 tuliyokuwa nayo mwaka jana hadi kufikia asilimia 85 ya uzalishaji, Nuru Kinamba amesema.
Aidha, Kindamba amebainisha kuwa kwa msimu wa 2025/2026 tunatarajia kutumia zaidi ya tani 8,400, ambazo zinatarajiwa kutuwezesha kufikia asilimia 92 ya uzalishaji.
Kwa upande wake Dodoma Hamabarage, mkulima wa ngano , amesema kabla ya mpango wa ruzuku, gharama za mbolea zilikuwa kubwa na kipato kilikuwa kidogo, lakini hali imebadilika baada ya kupata mbolea kwa bei nafuu.
“Mazao yameongezeka zaidi na kipato kimekuwa kikubwa, tunaweza hata kusomesha watoto.
Niwashauri wakulima wenzangu ambao hawajaanza kutumia mbolea waanze sasa, kwani inaleta tija kwenye uzalishaji.
Naye Samson Mwile, mkulima wa viazi, ameishukuru Serikali kwa elimu inayotolewa kupitia kampeni hiyo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na upimaji wa afya ya udongo. “Elimu hii italeta manufaa makubwa kwani tukijua aina ya udongo na mbolea zinazofaa tutazalisha kwa ufanisi zaidi,” amesema Mwile.
Kupitia juhudi hizo, Halmashauri ya Ileje inaendelea kuwa mfano wa utekelezaji bora wa sera za kilimo chenye tija nchini, ikiunga mkono dhamira ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya mwananchi mmoja mmoja kupitia kilimo.