UPIMAJI AFYA YA UDONGO NI NGUZO YA UZALISHAJI WENYE TIJA

Wakulima 127 wapimiwa Afya ya udongo na kupewa vyeti
Wakulima 127 kutoka Kijiji cha Utende, wilayani Mlele mkoani Katavi, wamepata elimu kuhusu umuhimu wa kulinda, kuboresha afya ya udongo kama msingi wa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhakikisha usalama wa chakula nchini baada ya mashamba yao kupimwa na kupewa vyeti kuhusu hali ya udongo.
Hayo yamezunguzwa katika Kijiji cha Utende, wilayani Mlele, mkoani Katavi, katika kampeni ya “Mali Shambani: Silaha Mbolea” inayolenga kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea, usajili wa wakulima kwenye mpango wa ruzuku na upimaji wa afya ya udongo, ambapo wakulima wamepewa elimu ya kisayansi kuhusu namna ya kuboresha rutuba ya udongo na kuongeza tija ya mashamba yao.
Akizungumza na wakulima, Afisa Kilimo wa Mkoa wa Katavi, Faridu Abdallah, alisema udongo wenye afya ni msingi wa kilimo endelevu na chanzo cha chakula bora.
“Afya ya udongo ndiyo moyo wa uzalishaji. Wakulima wakipima afya ya udongo na kutumia mbolea kwa sahihi, wataongeza mavuno na ubora ya mazao,” alisema Abdallah.
Abdallah aliongeza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na kilimo kisicho rafiki kwa mazingira vinaweza kudhoofisha udongo, hivyo kupunguza tija katika uzalishaji wa mazao.
Kwa upande wake, Daudi Palazi, mkulima wa nyanya kijijini Utende, alisema upimaji wa afya ya udongo umemsaidia kubaini virutubishi vinavyohitajika katika mashamba yake.
“Zamani tulikuwa tunatumia mbolea kwa mazoea, lakini sasa tumejua udongo wetu unahitaji nini. Mavuno yameongezeka na gharama zimepungua,” alisema Palazi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo , Bw. Samson Poneja, akimuwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, amekabidhi vyeti kwa wakulima waliokamilisha upimaji wa afya ya udongo na kusisitizwa kwenda kulima kwa kuzingatia matokeo ya afya ya udongo katika kuimarisha mashamba na kulinda mazingira.
“Kupima afya ya udongo ni hatua muhimu ya kisayansi inayosaidia kufanya maamuzi sahihi shambani. Tunawapongeza wakulima hawa kwa kuwa mfano wa kuigwa,” alisema Poneja.
Wakulima wanahimizwa kuendelea kupima afya ya udongo, kutumia mbolea kwa usahihi, na kusajili mashamba yao ili kuongeza tija na kuboresha uzalishaji.