Tfra Yaonya Wanaouza Mbolea Nje Ya Mfumo
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetoa onyo kali kwa wafanyabiashara wasio waaminifu pamoja na wakulima wanaonunua mbolea nje ya mfumo rasmi wa ruzuku kwa lengo la kuiuza kinyume na bei elekezi ya serikali au kuitorosha, ikisisitiza kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa kamwe.
Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, wakati wa hafla ya makabidhiano ya mifuko 320 ya mbolea sawa na tani 16 kwa vijana wa Wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Anasema upatikanaji wa kiasi hicho cha mbolea umewezeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, akizitaja kampuni zilizoshiriki kuwa ni pamoja na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), METL, ETG Inputs, Itracom, Minjingu, Mhema Agrovet na Jabiri Agrochemical na kuwashukuru kwa mchango wao katika kufanikisha upatikanaji wa pembejeo hizo.
Laurent anasema ruzuku ya mbolea ni jitihada mahsusi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuongeza tija ya kilimo, kuinua kipato cha mkulima na kukuza uchumi wa Taifa, huku vijana wakihimizwa kuichukulia sekta ya kilimo kama fursa ya ajira na maendeleo endelevu.
Kupitia kampeni ya “Mali Shambani, Silaha Mbolea”, TFRA inaendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha kilimo kinafanyika kwa misingi ya kisayansi.
Akizungumzia msimu wa kilimo wa 2025/2026, Laurent anasema mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani hadi wastani, hali inayowataka wakulima kutumia pembejeo sahihi kwa wakati na kwa viwango vinavyopendekezwa kitaalamu.
Anawapongeza wakulima wa Wilaya ya Makete kwa kuanza mapema msimu wa kilimo, hususan kwa mazao ya mahindi na viazi, akisema hatua hiyo inaonesha utayari wa wilaya hiyo kuchangia katika usalama wa chakula na uzalishaji wa mazao ya biashara nchini.
Kwa vijana waliokabidhiwa mbolea, Laurent anahimiza zitumike kwa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu na mashamba yao yatumike kama mashamba darasa kwa wakulima wengine.
Aidha, anawahakikishia wananchi kuwa mbolea zipo za kutosha nchini, huku viwanda vya ndani vikiendelea kuzalisha na kusambaza mbolea, na kupongeza uongozi wa Mkoa wa Njombe, Wilaya ya Makete pamoja na wadau wote kwa kushirikiana kuhakikisha sekta ya kilimo inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Kissa Kasongwa, anasema uwezeshaji wa vijana ni ajenda ya kudumu ya uongozi wake, akibainisha kuwa mpango wa ugawaji mbolea unaendana kikamilifu na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwasaidia vijana kujitegemea kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
Kasongwa anaishukuru TFRA kwa kubeba jukumu hilo kwa kiwango kikubwa, akisema Mamlaka hiyo imeonesha dhamira ya dhati katika kuboresha sekta ya kilimo Wilaya ya Makete.
Aidha, anatoa shukrani kwa Wizara ya Kilimo na kueleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Makete inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kukuza kilimo hususan kwa vijana, kwa lengo la kuongeza ajira na kipato.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samuel Mshote, anasema ongezeko la matumizi ya mbolea nchini linachangiwa kwa kiasi kikubwa na elimu inayotolewa kupitia kampeni ya “Mali Shambani, Silaha Mbolea,” akibainisha kuwa TFC itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo muhimu kwa wakulima kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Akizungumza kwa niaba ya vijana na watu wenye ulemavu walionufaika na mpango huo, Noadi Tweve anatoa shukrani kwa msaada wa pembejeo uliotolewa, huku akihamasisha wilaya nyingine kuiga mfano wa Makete kwa kuwashirikisha vijana na watu wenye mahitaji maalum katika miradi ya kilimo amesema, jitihada hizo zimeacha alama ya kudumu kwa walionufaika.
