WAZIRI WA KILIMO AONYA WANAOHUJUMU MCHAKATO WA MBOLEA ZA RUZUKU
WAZIRI WA KILIMO AONYA WANAOHUJUMU MCHAKATO WA MBOLEA ZA RUZUKU
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ametoa onyo kali kwa mawakala wanaojihusisha na uchanganyaji wa mbolea bandia, akisisitiza kuwa serikali ipo macho na itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kuhujumu zoezi la mbolea za ruzuku.
Waziri Chongolo ametoa kauli hiyo wakati akishuhudia uzinduzi wa ghala la mbolea litakalohudumia mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Amesema, serikali haitamvumilia mtu au kikundi chochote kitakachoharibu mchakato wa usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, amesema hadi sasa jumla ya tani milioni moja za mbolea zimetumika nchini, ambapo asilimia 80 ya tani hizo zimeagizwa kutoka nje ya nchi.
Joel ameongeza kuwa, TFRA itaendelea kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara wa pembejeo ili kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora zinazowasaidia wakulima katika misimu yote ya kilimo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Wazo Mwang'onda, ameipongeza TFRA pamoja na mawakala wa pembejeo wa Njombe kwa kusimamia vizuri mchakato wa upatikanaji na usambazaji wa mbolea kwa wakulima.
Amesema, sekta ya kilimo mkoani Njombe inaendelea kuvutia kutokana na wakulima wengi kutumia mbolea, hali inayochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao.
Aidha, amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwasaidia wakulima kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija zaidi.
Baadhi ya mawakala wa pembejeo wamesema uzinduzi wa ghala hilo mjini Makambako ni fursa muhimu kwa wakulima wa mikoa ya kusini, ikizingatiwa kuwa maeneo hayo ndiyo tegemeo kubwa la uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Mhema Zuku Agro amesema kupitia shughuli za usambazaji wa pembejeo, zaidi ya vijana 300 wameajiriwa na kupatiwa mafunzo, jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali.
Amesema, Katika ghala hilo, zaidi ya tani 3,000 za mbolea zitakazoagizwa moja kwa moja kutoka nje ya nchi kupitia wafanyabiashara wa pembejeo wa mkoani Njombe zitspatikana muda wote.
