Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
USHIRIKIANO WA WADAU WATAJWA KUONGEZA TIJA YA UZALISHAJI MAZAO YA KILIMO
16 Jul, 2026
USHIRIKIANO WA WADAU WATAJWA KUONGEZA TIJA YA UZALISHAJI MAZAO YA KILIMO

Imeelezwa kuwa, zao la ufuta ni miongoni mwa mazao yanayohitaji matumizi makubwa na sahihi ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuboresha ubora wa mavuno.

Mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ametoa maelezo hayo mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, alipotembelea banda hilo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Amebainisha kuwa, wakulima wengi wa kusini mwa Tanzania hufanya kilimo cha kuhamahama kutafuta maeneo yenye rutuba badala ya kutumia mbolea kutokana na mazoea ambapo wakitumia mbolea kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu wataongeza uzalishaji wa zao hilo pamoja na kuongeza thamani yake bila kuadhiri eneo la makuzi ya watoto kutokanako na kuhamahama.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali yaliyoshiriki maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji, Laurent, amesema ushirikiano miongoni mwa taasisi za utafiti, sekta binafsi na wadau wa kilimo ni msingi muhimu katika kuimarisha matumizi sahihi ya mbolea, kuongeza uwekezaji na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Laurent amesema TFRA itaendelea kushirikiana na TARI katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kimkakati, ikiwemo ufuta.

Katika banda la Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), Meneja wa Mradi wa taasisi hiyo, Peter Mwangalo, amemueleza Laurent kuhusu juhudi zinazofanywa katika  kuhamasisha kilimo endelevu na matumizi ya mbolea za asili. 

Laurent ameipongeza SAT kwa mchango wake wa kutoa elimu kwa wakulima na kusisitiza kuwa, TFRA iko tayari kuimarisha ushirikiano na taasisi hiyo pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea za kiorganiki.

Aidha, alipotembelea banda la TPHPA, Laurent amepata maelezo kutoka kwa Mbalamwezi Hussein kuhusu tofauti kati ya mbolea za maji na viuatilifu. 

Ameelezwa kuwa, mbolea hutoa virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji wa mimea, wakati viuatilifu ni sumu iliyoandaliwa maalum kwa ajili ya kudhibiti wadudu na magonjwa yanayoshambulia mazao.

Naye Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Franley Mngumi, amesema ushirikiano kati ya TFRA na Tume hiyo umefungua fursa kwa vyama vya ushirika kushiriki katika biashara ya mbolea na kuwafikishia wakulima huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.

Ziara ya Laurent imehitimishwa katika banda la Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), ikiwa ni sehemu ya juhudi za TFRA za kuimarisha ushirikiano na wadau wa tasnia ya mbolea kwa lengo la kuimarisha mashirikiano ili kuwahudumia wakulima nchini kwa weledi na juhudi kubwa.