Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
WAZIRI BASHE AZINDUA UGAWAJI WA VISHIKWAMBI 3500 KURAHISISHA USAJILI WA WAKULIMA
30 May, 2024
WAZIRI BASHE AZINDUA UGAWAJI WA VISHIKWAMBI 3500 KURAHISISHA USAJILI WA WAKULIMA

Wizara ya Kilimo imeazimia kuhakikisha kuwa miradi ya kilimo inatekelezwa ipasavyo ili kuweza kumnufaisha mkulima na kufikia lengo la Serikali la kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 10 huku ikilenga kufikia bilioni 2.3 ya mauzo ya mazao katika nchi za nje.



Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) tarehe 7 Mei, 2024 katika hafla ya Uzinduzi wa Ugawaji wa Vishikwambi na POS Kwa Maafisa Ugani Kilimo na Mawakala wa Pembejeo za Kilimo Mtumba, jijini Dodoma ambapo vishikwambi 3500 pamoja na POS vitarahishisha usajili wa wakulima katika mifumo ya ugawaji wa pembejeo na upimaji wa afya ya udongo.



Aidha, Waziri Bashe amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha miradi yote ya Kilimo inatekelezwa ipasavyo akiwataka Viongozi hao kuwa na Mamlaka ya kusimamia watumishi wa Wizara katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu waliyopewa.



Waziri Bashe amesema kuwa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kilimo utaondoa changamoto ya wizi na kukosekana kwa uwajibikaji katika miradi ya kilimo.



Naye Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela amempomgeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuiheshimisha Sekta ya Kilimo kupitia ongezeko la bajeti kutoka bilioni 970.8 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia trilioni 1.24 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.



Mhe. Shigela amesema ni lazima tuizingatie Sekta yenye watu wengi nchini akitaja Sekta ya Kilimo kama Sekta yenye asilimia 80 ya Watanzania.



Akiwasilisha salamu za Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amewataka wananchi kubadili mitazamo yao na kujikita katika kilimo ili waweze kunufaika na uzalishaji kupitia miradi ya umwagiliaji yenye thamani ya takribani shilingi billion 146 ambayo imewekwa katika Mkoa huo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Bw. Joel Laurent amesema upatikanaji wa mbolea nchini umeongezeka kutoka tani 766,000 mwaka 2021 hadi kufikia tani 1, 035,000 mwaka 2024.


Bw. Joel ameeleza kuwa ongezeko la upatikanaji huo wa mbolea nchini umuchangiwa na ongezeko la uzalishaji wa ndani kutoka asilimia 6 ya mahitaji mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11 mwaka 2024 pamoja na uingizaji wa pembejeo hiyo muhimu kutoka nje ya nchi.



Hafla hiyo imehudhuriwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu Wizara ya Kilimo na Tamisemi, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi wya Idara/Vitengo, Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Wawakilishi wa Serikali.