TFRA Yatangaza Mafunzo Bure ya Leseni za Uuzaji Mbolea kwa Wakulima Rorya
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetangaza fursa ya kutoa mafunzo bure kwa wakulima na wananchi wanaotaka kuanzisha biashara ya mbolea katika vijiji vya Tatwe, Nyamusi na Panyakoo vilivyopo Wilaya ya Rorya, mkoa wa Mara.
Hayo yamezunguzwa leo tarehe 11 Desemba, 2025 wakati wa kampeni ya Mali Shambani na , Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi kutoka TFRA, Godwin Vedastus alisema
Mamlaka imeamua kutoa mafunzo ya mbolea bure ili kumwongezea mkulima upatakanaji wa mbolea karibu na makazi yake. Mtu yeyote anayehitaji kuingia katika biashara ya mbolea anakaribishwa kupata leseni bila gharama yoyote ya mafunzo,” alisema Vedastus.
Kwa upande wake, Afisa Masoko kutoka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Shafi Omary, alisema kuwa kampuni hiyo imeweka masharti nafuu kwa mawakala wapya ili kuongeza mtandao wa usambazaji wa mbolea nchini
“TFC inasajili mawakala kwa kianzio cha mifuko 20 pekee, na kwa mawakala wa vijijini hata nusu tani inakutosha kuwa wakala rasmi,” alisema Omary.
Naye Afisa Mawasiliano na Masoko kutoka kampuni ya Minjingu Fertilizers Ltd, Kisuma Mapunda, alisema kuwa kampuni hiyo pia imefungua milango kwa wakulima wanaotaka kuingia kwenye biashara ya mbolea kwa masharti rahisi.
“Kwa Minjingu, kuwa wakala kunahitaji kianzio cha kuanzia shilingi 500,000 tu. Tumepunguza gharama ili kuwapa nafasi vijana na wakulima kuingia kwenye biashara hii,” alisema Mapunda.
Kupitia fursa hizi, wakulima wa Rorya wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa mbolea kwa urahisi na kufungua milango ya vijana na wajasiriamali kukua kiuchumi, ikichochea ongezeko la mawakala wapya na kuboresha mnyororo mzima wa usambazaji wa pembejeo za kilimo hasa kwa mkoa wa Mara.
