Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

WATUMISHI TFRA wapewa elimu ya mipango, usimamizi wa fedha na uwekezaji


Tunapoelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa tarehe 8 Machi, 2024 kila mwaka, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewajengea uwezo katika eneo la fedha watumishi wake ili kuwakumbusha kujiwekea akiba na kuwekeza kusikohitaji nguvu kubwa.Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam zilipo ofisi za Mamlaka baada ya wanawake wengi kuhitaji elimu ya fedha iliyopelekea uongozi wa Mamlaka kuridhia na kumuandaa mwezeshaji wa masuala hayo.Mkurugenzi wa TFRA, Joel Laurent ametaka mafunzo hayo yawasaidie watumishi hao kuwa na fikra chanya ya kuweza kufikia dhana ya usawa kama inavyoshauriwa na viongozi wa kitaifa na kimataifa."Tuwe tunajiuliza endapo kuna mahala tunaona tumelala kidogo katika masuala ya kijinsia basi tuamke" amesema Laurent.Ameeleza kuwa, ili mtu yeyote aweze kuwekeza anahitaji kuwa na uelewa juu ya namna ya kuwekeza hususan uwekezaji unaohusisha kununua hisa, kuweka amana, hatifungani na uwekezaji mwingine wote ili uweze kunufaika.Akitoa mafunzo hayo, Mwezeshaji CPA, Emmilian Busara amesema ajira ni nzuri lakini zina ukomo na kuwakumbusha umuhimu wa kuwekeza na kuweka akiba itakayowawezesha kuendesha maisha yao mara baada ya ajira kukoma au kukutana na jambo litakalowatoa kwenye ajira.CPA Busara, amewataka watumishi kuweka malengo ya juu katika mipango yao huku akifafanua kuwa mafanikio ya mtu yanatokana na kile anachokusudia kukipata moyoni mwake, pia aliwashauri kuwa na vyanzo tofauti vya mapato ili kimoja kikisumbua unakuwa na uhakika wa kuingiza kipato kupitia chanzo kingine na hivyo kupunguza msongo wa Mawazo."Huwezi kufanikiwa zaidi ya unavyowaza, jitahidi kuwaza mambo makubwa maana huwezi kufanikiwa zaidi ya unavyowaza" Busara alisisitiza.Naye Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Victoria Elangwa aliwataka watumishi kuyaingiza mazuri waliyojifunza kwenye matendo na si kuyatia kapuni, amesema watumishi wamehamasika sana kwa elimu waliyoipata na kuwashauri vijana waliobahatika kujifunza elimu ya uwekezaji katika umri mdogo kutumia fursa hiyo itakayowapa uhuru wa kifedha katika Maisha yao.Mwisho aliwataka watumishi ambao umri wa kati kutumia elimu hiyo kuanzia hapo walipo na kueleza itasaidia kubadilisha masuala fulani ya namna fedha yao inavyotumika kwa kuwekeza zaidi.