Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Wanufaika elimu ya matumizi sahihi ya mbolea watakiwa kuwa mabalozi
29 May, 2024
Wanufaika elimu ya matumizi sahihi ya mbolea watakiwa kuwa mabalozi

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), DKt. Stephan Ngailo amewataka viongozi na wana vikundi vya wakulima mkoa wa Lindi kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya mbolea kwa kilimo chenye tija.

Dkt. Ngailo ametoa wito huo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kukagua mashamba ya mfano yaliyolenga kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea bora kwa wakati kwa shughuli za kilimo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Aidha, Dkt. Ngailo amewataka wakulima wa mazao ya mahindi kufuata kanuni zote za kilimo ikiwa ni pamoja na kuchagua shamba, kuandaa shamba kwa wakati, kupanda kwa kutumia mbolea sahihi ya kupandia na kwa wakati, kuweka mbolea ya kukuzia na kupalilia kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo akisikiliza maelezo ya Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhusiano, Mawasiliano na Elimu kwa Umma Matilda Kasanga juu ya shamba darasa lililolimwa kwa kutumia mbolea na lile ambalo halikutumia mbolea alipofanya ziara katika kijiji cha Chimbila B Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi

"Shamba likifuata kanuni zote za kilimo huwa na matokeo mazuri na hivyo kuongeza tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla" Dkt. Ngailo alisisitiza.

Dkt. Ngailo aliongeza kuwa, kufuatia kutokuwepo kwa matumizi ya mbolea kwa wakulima katika mikoa ya Lindi na Mtwara, mamlaka iliona vyema kufanya uhamasishaji kwa njia ya kuanzisha mashamba ya mfano ambayo vikundi vya wakulima vinashiriki kikamilifu kuanzia msimu wa kupanda mpaka msimu wa mavuno ili kujionea kila hatua zi avyokwenda na kupata ujuzi.

Pamoja na kuanzisha mashamba ya mfano mamlaka imewawezesha wanakikundi mmoja mmoja kwa kuwapa mbolea ili kwenda kutumia kwenye mashamba yao binafsi ili kwa njia hiyo wananchi wengine waweze kujifunza na kuhamasika kutumia mbolea.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa mashamba darasa na namna elimu inavyotolewa kwa wakulima wakati wa ziara hiyo, bibi shamba Eva Kachime alisema mpaka Machi 2022 wamewafikia wakulima 51 na miongoni mwao wakulima 11 wamehamasika kutumia mbolea.

“Tunaamini wakulima wa Mnacho wakihamasishwa kutumia mbolea mkoa wa Lindi utakuwa umejikomboa na kuondokana na changamoto ya njaa pia kipato cha mkulima mmoja mmoja kitaongezeka na kupunguza umaskinikwa wana Ruangwa” alisema kachime.

Pamoja na hayo, Kachime aliishukuru serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kuanzisha mashamba ya mfano katika kata anayoisimamia na kueleza kuwa wakulima wamehamasika na kuona utofauti mkubwa kati ya shamba lililopandwa kwa mbolea na lisilotumia mbolea.

Aidha, ameiomba serikali kuendelea kutoa hamasa kwa kipindi cha miaka 3 mfululizo ili kuwafikia wakulima wengi zaidi na hivyo kuisaidia jamii kuachana na kilimo cha asili wanachokitaja kama kilimo bibi ambacho hakitumii mbolea.

Alisema, kata ya Mnacho ni kata inayotegemewa kwa kuzalisha chakula kwa wingi hivyo uhamasishaji wa mbolea utaongeza tija zaidi.

Kwa upande wake, Said Mnangona Afisa kilimo Kata ya chigugu Masasi DC alieleza kuwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea imeongeza tija kwake na kwa wakulima wengine kwani katika heka moja na nusu aliyolima anamatarajio ya kuvuna gunia 30 za mahindi tofauti na awali alipokuwa akivuna chini ya gunia nane za mahindi.

Mzee Rashid Mandumba mwanakikundi wa jitegemee anasema awali alikuwa hatumii mbolea kulingana na desturi na mazoea na kukiri kuwa uhamasishaji wa matumizi ya mbolea umeleta tija kwake na kwa jamii yake kwa ujumla.

Alisema, matumizi ya mbolea yanawasaidia kulima eneo dogo lakini wanapata matokeo na kipato kikubwa kuliko kulima eneo kubwa bila mbolea na kuambulia hasara pamoja na kupoteza nguvu.

Ziara hii ni hatua ya maandalizi kuelekea siku ya mkulima yenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea inayotarajia kufikia kilele mwezi Aprili 2022 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.