Wakulima wa korosho washauriwa kutumia mbolea kuongeza tija

Katika kuhakikisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea inawafikia wakulima wote nchini, leo tarehe 30 Julai, 2022 imeshiriki kwenye mbio za korosho ( Korosho marathony) zilizoanza na kuishia katika kiwanja cha Nangwanda sijaona mkoani Mtwara.
Akizungumza katika banda la maonesho kiwanjani hapo mara baada ya kumaliza mbio hizo, Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka, Victoria Elangwa amesema ushiriki wa TFRA ni muhimu kwani unawafanya wananchi kufahamu uwepo na majukumu yanayosimamiwa na mamlaka hiyo kisheria.
Pamoja na uwakilishi wa Mkurugenzi Elangwa, TFRA iliwakilishwa na wadhibiti ubora wa mbolea, Allan Marik na Azizi Mtambo, Afisa Biashara, Daniel Maarifa na Mtaalam wa maabara, Godluck Christian.
Akizungumza na wananchi waliotembelea banda la maonesho lililokuwa katika viwanja hivyo, Allan Marik amesema majukumu ya Mamlaka ni pamoja na kuhakikisha wakulima nchini wanapata na kutumia mbolea bora zilizodhibitishwa kwa matumizi ya kilimo.
Ameongeza kuwa, jukumu jingine ni pamoja na kusajili mbolea zinazozalishwa nchini pamoja na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ili kuwafanya wakulima kutumia mbolea sahihi kwa kilimo chenye tija, kusajili wafanyabiashara wa mbolea nchini.
Kwa upande wake Azizi Mtambo amewashauri wananchi na wakulima wa korosho na mazao mengine kutumia mbolea kwenye kilimo cha korosho ili kuongeza uzalishaji na hivyo kuongeza usalama wa chakula na tija kwa uchumi wao na taifa kwa ujumla.