Elimu ya Mbolea Yabadili mtazamo wakulima Meatu
Wakulima wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu wamebadilisha mtazamo baada ya kupata mafunzo yaliyowapelekea kufahamu kuwa mbolea si chanzo cha uharibifu wa udongo, isipokuwa ni nyenzo muhimu ya kuuwezesha udongo kurudisha uhai wake na kuchochea uzalishaji.
Hayo yamebainishwa na wataalam wakati wa kampeni maalum ya Mali Shambani inatotekelezwa na Wizara ya Kilimo na taasisi zake kuelekea msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Newaho Mkisi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka nguvu katika kuboresha sekta ya kilimo nchini hasa kwa kuweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo hususan mbolea na mbegu.
Mkisi amesema kuwa, mahitaji ya mbolea wilayani humo yameongezeka sana tofauti na ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita. Ameeleza kuwa, sasa wakulima wanaelewa kuwa mbolea si adui wa udongo bali ni kirutubisho muhimu katika ukuaji wa mmea.
"Naipongeza TFRA kwa kuhakikisha mbolea zinazopatikana sokoni ni salama na zinakidhi mahitaji ya wakulima", Mkisi ameongeza.
Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Godwin Vedatus, ameeleza kuwa, ili mimea ikue vizuri na kupata virutubisho muhimu, matumizi ya mbolea ni ya msingi.
Amesema, udongo unapochoka, ni muhimu kurejesha virutubisho kwa kutumia mbolea ili kuimarisha ustawi wa mazao.
“Mbolea haiharibu udongo. Kinyume chake, inauongezea virutubisho ambavyo mimea inahitaji ili kustawi kwa afya na uzalishaji wenye tija.” Ameongeza.
Aidha, mkulima Masanja Nkobadi ametoa wito kwa wakulima wenzake na kueleza kuwa dhana ya kwamba mbolea inaharibu udongo imekuwa ikiwadanganya kwa muda mrefu. “Sisi Wasukuma tumekuwa tukijidanganya.
Mimi nimetumia mbolea na nimepata mavuno mengi"
Amewasihi wakulima kutumia mbolea kwani inaongeza tija.
