Wakulima Madibila waeleza tija iliyotokana na Mbolea ya ruzuku 2022/2023

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwila ameeleza kuwa, wilaya yake ni miongoni mwa wilaya zenye matumizi makubwa ya mbolea na kushukuru kwa ruzuku ya mbolea inayotolewa na Serikali ya Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkuu wa Wilaya, Mwila ameeleza hayo mbele ya wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Anthony Diallo waliopowatembelea na kuzungumza nao kwa lengo la kujifunza, kusikiliza na kupokea maoni yao.
Akizungumza kwa niaba ya wanaushirika wa Madibira Agricultural Marketing Co-operative Society LTD (MAMCOS LTD) Afisa Kilimo na Umwagiliaji wa Skimu ya Umwagiliaji ya Madibila iliyoko Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Hagai Efrahim Kisunga amesema mbolea ya ruzuku imeongeza tija kubwa sana kwa msimu uliopita wa kilimo.
Amesema, kabla ya mtikisiko wa bei za mbolea wakulima katika skimu hiyo walikuwa wakivuna kiasi cha tani 7.5 hadi 8 kwa hekta na baada ya bei ya mbolea kupanda kwenye soko la dunia wakulima walishindwa kumudu bei ya mbolea na kutumia mifuko mitatu hadi minne badala ya mifuko ya mbolea 8 hadi 9 ya kg 50 kwa hekta moja na kupelekea kushuka kwa uzalishaji na tija ambapo walizalisha tani 4.5 hadi 5 tu za mpunga.
Ameeleza kuwa, baada ya Serikali kuweka ruzuku ya mbolea msimu wa kilimo 2022/2023, wakulima waliweza kununua mbolea na kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya zao na hivyo kwa msimu uliopita wa kilimo wakulima wameweza kunufaika na kuzalisha tani 7.5 hadi 8 kwa hekta na hivyo kupata faida kubwa kwenye kilimo cha mpunga.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo ameutaka uongozi wa chama hicho kuhakikisha wanachama wake wote wamejisajili katika daftari la mkulima na baadaye kwenye mfumo wa kidigitali wa mbolea ya ruzuku ili waweze kunufaika na mpango huo wa mbolea za ruzuku unaotolewa na Serikali.
Aidha, amewataka kuwahudumia wakulima wengine wasio wanachama ili kuisaidia Serikali kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima wa pembezoni
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi, Patrick Mwalunenge alitaka kujua mchakato uliokuwa ukitumiwa na ushirika huo kupata mbolea na kuwasambazia wakulima wao na kuelezwa mwaka 2021 walitumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja na wao walikuwa wakiwasilisha mahitaji yao TFRA waliohusika kuagiza mbolea nje ya nchi na kuifuata baada ya kiasi walichokiomba kufika nchini na kuisambaza kwa wakulima wao.
Ameeleza kwa sasa chama chao kimejisajili ili kushiriki kwenye usambazaji wa mbolea za ruzuku na kueleza tayari wameshiriki mafunzo yaliyotolewa na TFRA ikiwa ni kigezo cha kushiriki kwenye mpango huo ambapo wanasubiri cheti ili kukamilisha taratibu za usajili na kupata namba ya uwakala