Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Wakulima Lindi watakiwa kufuata ushauri wa kitaalam
09 Sep, 2024
Wakulima Lindi watakiwa kufuata ushauri wa kitaalam

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuachana na maneno ya kusikia kutoka kwa watu wanaowaaminisha kuwa mbolea inaharibu udongo badala yake wafuate ushauri unaotolewa na wataalam wa kilimo ikiwemo kutumia mbolea kwa usahihi kwenye shughuli zao za kilimo.

Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni inayotekelezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ya Kilimo ni mbolea uliofanyika katika kijiji cha Mandawa wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi yenye lengo la kuwaelimisha wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha usajili wa wakulima kwenye mfumo wa kidijitali wa mbolea za ruzuku.

"Wananchi tubadilike yapo maneno yanasema ukitumia mbolea unaharibu udongo, mbolea ingekuwa inaharibu udongo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wanaolisha nchi nzima nasisi tukiwepo wasingekuwa wanazalisha mpaka sasa".

Hayo maneno tunayoyaamini kutoka kwa watu wasiokuwa na utaalam, hawajaenda shule tuachane nayo, tunatumia nguvu kubwa ya kulima eneo kubwa wakati matumizi ya mbolea yangetufanya tulime eneo dogo kwa matokeo makubwa" Nyundo alisisitiza.

"Sisi tunao maafisa kilimo kwenye ngazi ya Mkoa, Wilaya, kata na vijiji na maafisa hao wanaujuzi unaofanana na wale wa wizarani n awa taasisi, hivyo niwaombe wakulima watumieni maafisa hao ili wawashauri namna bora ya kuendesha shughuli za kilimo kwa tija " Nyundo aliongeza.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Robert Mtendamema ametoa shukrani kwa uongozi wa Mkoa na wilaya kwa kushirikiana kikamilifu katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kupitia kampeni hiyo.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya kilimo imekusudia Sekta ya kilimo kukua kwa asilimia kumi ifikapo mwaka 2030 na kueleza matumizi sahihi ya mbolea yatachangoza kufikiwa kwa lengo hilo kwani wakulima watazalisha kwa tija na kuongeza vipato vyao na taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa, Farida Kikoleka amesema, huko nyuma suala la kilimo lilikuwa kama adhabu ila kwa sasa wananchi wamebadilika na wanajua kuwa kilimo ni chakula lakini pia wanajua kilimo ni biashara.

Kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi kuhudhuria hafla hiyo amewataka kuwa mabalozi wa kufikisha ujumbe na elimu ya mbolea waliyoipata kwa wakulima waliokosa fursa hiyo.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kilwa, Mbaruku Masudi ameipongeza TFRA kwa kuja na wazo na kuamua kushuka hadi ngazi ya wakulima ili kuwapa elimu muhimu ya mbolea.

Ameiomba Mamlaka kuwa na nia ya kuwafikia wakulima wa kata nyingine takribani 22 ambao hawakufanikiwa kushiriki hafla hiyo ya uzinduzi.

Mbolea Day