Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Vituo vya kuuzia mbolea vyaongezeka kutoka 27 hadi 80 Tabora
29 May, 2024
Vituo vya kuuzia mbolea vyaongezeka kutoka 27 hadi 80 Tabora

Mkoa wa Tabora umeongeza vituo vya kuuzia mbolea kutoka vituo 27 msimu wa kilimo 2022/2023 hadi vituo 80 mwaka 2023/2024 ili kumaliza changamoto ya wakulima kutembea umbali mrefu kufuata bidhaa hiyo.



Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi, Dkt. Batilda Burian, tarehe 08 Oktoba, 2023 alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya uwepo wa maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yatakayofikia kilele chake tarehe 13 Oktoba, 2023.



Alisema kufanyika kwa maadhimisho hayo ndani ya mkoa huo kunatoa fursa kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo mkoani Tabora na mikoa jirani ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Kilimo.



Alieleza kuwa, katika Maadhimisho hayo, wataalam mbalimbali kutoka taasisi za utafiti, kampuni za mbolea, vyuo vikuu, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa kilimo watapata fursa ya kutoa elimu kwa wakulima ikiwemo elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, matumizi sahihi na salama ya viuatilifu, afya ya udongo, matumizi ya mbegu bora na udhibiti wa tasnia ya mbolea kwa ujumla.



Dkt. Batilda alibainisha kuwa, pamoja na elimu itakayotolewa katika maadhimisho hayo, kutakuwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali za wakulima kwa tarehe 11 na 12 Oktoba,2023 ikiwemo pembejeo za mbolea, mbegu na viuatilifu zitakazooneshwa na makampuni zinazouza pembejeo hizo hapa nchini.



Alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni Agenda 10/30: Matumizi Sahihi ya Mbolea ya Ruzuku kwa Kilimo chenye Tija kauli ambayo imebeba ujumbe wenye matumaini mapana kwa wakulima.



Aidha, Dkt. Batilda alimshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa mbolea ya ruzuku na kuinua wakulima wote nchini.



“Tunamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga shilingi bilioni 150 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ili kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima lengo likiwa kuwapunguzia makali”, Dkt. Batilda alisema.



RC aliongeza kuwa kupitia rukuzu hiyo Mkoa ulipokea na kutumia zaidi ya tani 8,000 za mbolea zenye thamani ya shilingi bilioni 8.5 kwa msimu wa kilimo 2022/2023 ambapo jumla ya wakulima 29,517 walinufaika na mbolea hiyo.



Mwisho, Mkuu wa Mkoa Balozi, Dkt. Batilda alitoa wito kwa wakulima na wadau wote wa sekta ya kilimo kushiriki katika maadhimisho hayo ili kujifunza teknolojia mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Kilimo.