Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
UZALISHAJI WA NDANI WA MBOLEA KUONGEZEKA
11 Jul, 2024
UZALISHAJI WA NDANI WA MBOLEA KUONGEZEKA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania  (TFRA) imesema kuwa uzalishaji wa ndani wa mbolea utaongezeka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu   na hivyo kutosheleza mahitaji ya soko ya   pembejeo hiyo muhimu.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Antony Diallo, Jijini Dar es Salaam, alipotembelea banda la Mamlaka kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea.

Dkt. Diallo amesema, Agenda 10/30: Kilimo ni biashara inatutaka ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe na uwezo wa kujitosheleza kwa mbolea pamoja na kuuza nchi jirani kutokana na uwepo wa viwanda vinavyotosheleza mahitaji ya nchi.

"Siyo tu kusubiri mwaka 2030 kwasasa tumeshaanza kuzalisha kiwango kikubwa cha mbolea nchini na tunatarajia hadi mwisho wa mwaka huu (2024) tutakuwa na uwezo wa kuzalisha kiwango chote cha mahitaji yetu," Dkt. Diallo alisema.

Alisema, kwa sasa upatikanaji wa mbolea nchini unafikia asilimia 80 hadi 90 na kwamba mahitaji ni takribani tani 850,000 na yanaelekea kufikia tani milioni moja ambazo zinaweza kuzalishwa nchini.

Amesema, fursa za kuwekeza nchini ni nyingi zinazoendana na upatikanaji wa malighafi  zinazoweza kutumika kuzalisha mbolea nchini.

Kufuatia hilo, ni vyema Mamlaka kutangaza fursa hizo muhimu ili kupata wawekezaji watakaowekeza kwenye viwanda vya mbolea na hivyo kuisaidia nchi kuondokana na utegemezi.

Dkt. Diallo amesema maonesho hayo ni muhimu kwasababu watu kutoka mataifa mengine wanafika na hivyo kutupa fursa ya kupata wanunuzi wa mbolea zinazozalishwa Tanzania.

Mwisho, Dkt. Diallo ametoa wito kwa Watanzania kutembelea banda hilo ili kupata elimu ya shughuli zinazosimamiwa na Mamlaka  kwa maslahi ya sekta ya kilimo na Taifa kwa ujumla.

Mbolea Day