Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Utegemezi wa mbolea nje ya Afrika wapelekea matumizi hafifu, uzalishaji mdogo
29 May, 2024
Utegemezi wa mbolea nje ya Afrika wapelekea matumizi hafifu, uzalishaji mdogo

Imeelezwa kuwa, mbolea nyingi inayotumika Afrika inatoka nje ya bara hilo, wakati ile inayotengenezwa Afrika inauzwa nje ya bara hilo.



Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akizungumza kando ya mkutano wa Mifumo ya Chakula Barani Afrika wakati wa majadiliano kuhusu ajenda ya mbolea Barani Afrika na afya ya udongo iliyofanyika katika ukumbi wa Selous ndani ya jengo la mikutano ya kimataifa la Julius K. Nyerere Jijini Dar Es Salaam.



Waziri Mkuu mstaafu Pinda alisema, zaidi ya asilimia 90 ya mbolea nchini inaagizwa kutoka nje huku chini ya asilimia kumi ikitengenezwa ndani ya nchi.



Aliongeza kuwa, kwa sasa mbolea inayopatikana nchini inatoka nchi mbalimbali ikiwemo Russia, na kwa sasa upatikanaji wake umekuwa na changamoto kutokana na vita inayoendelea katika nchi hiyo.



Pinda aliongeza kuwa, hali hiyo imesababisha bei ya mbolea kupanda na pia mbolea kuadimika na kufikia kuhatarisha usalama wa chakula kwa baadhi ya nchi za Afrika.



Aliongeza kuwa, kutokana na bei ya mbolea kupanda duniani, Serikali za nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania zimeanzisha programu wezeshi za kusaidia upatikanaji wa mbolea ili kuleta suluhu ya changamoto hiyo kwa kuweka ruzuku kwenye pembejeo hiyo.



Kwa upande mwingine Pinda alisema matumizi ya mbolea yasiyofaa yamechangia kuendelea kuzorota kwa afya ya udongo na kusababisha mavuno kuwa hafifu.



Akizungumza alipokuwa akikaribisha mjadala kuhusu tasnia ya mbolea na afya ya udongo Rais wa Agra Afrika Dr. Agness Kalebata alisema asilimia hamsini (50%) ya chakula kinacholiwa duniani kinazalishwa kwa kutumia mbolea.



Akaongeza kuwa, matumizi ya mbolea yameendelea kuwa hafifu kutokana na upatikanaji wake kuwa mdogo na hivyo kupelekea uzalishaji mdogo wa mazao.



Akizungumza wakati wa majadiliano mmoja wa Pannelist alieleza kuwa, bara la Afrika linahitaji kuongeza uzalishaji wa mbolea ili kupunguza utegemezi kutoka nchi zilizoendelea na hivyo kutuhakikishia afya bora ya udongo unaotumika katika kuzalisha mazao.



Aliongeza kuwa, udongo unahitaji virutubisho kama vile mwili wa mwanadamu unavyohitaji ili uendelee kuzalisha na kuleta tija kwa wakulima.



Imeshauriwa serikali mbalimbali barani Afrika kufanya kazi bega kwa bega na taasisi binafsi ili kutatua changamoto ya pembejeo ya mbolea.



Kufanya kazi, kuboresha mbegu na kuhakikisha mbolea bora inapatikana kwa wakati sahihi na mahala sahihi kutawawezesha wakulima kuzalisha kwa tija na kuinua vipato vyao