Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Serikali yasaini Hati ya Makubaliano na kampuni ya Essa ya nchini Indonesia
02 Aug, 2024
Serikali yasaini Hati ya Makubaliano na kampuni ya Essa ya nchini Indonesia

Katika kukabiliana na uhaba na utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) wamesaini Hati ya Makualiano (MoU) na Kampuni ya ESSA ya nchini Indonesia iliyoonesha nia ya kuwekeza kwenye kiwanda cha kuzalisha mbolea.
Kampuni hiyo inatarajia kuanza ujenzi  wa kiwanda kitakachokuwa kikizalisha mbolea aina ya UREA kwa kutumia gesi asilia, kitakachojengwa mkoani Mtwara na kutarajiwa kuchangia katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, ajira kwa vijana pamoja na faida  nyingine za kiuchumi na kijamii.

Makubaliano hayo yameingiwa tarehe 31 Julai, 2024 katika hoteli ya Hyatt Dar es Salaam, the Kilimanjaro ambapo ilielezwa ujenzi wa kiwanda unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwaka 2027 na uzalishaji wake kuanza miaka miwili baadaye yaani 2029.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, Waziri wa Mipango na uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema, ujenzi wa kiwanda hicho utaifanya Tanzania kujitegemea kwa asilimia 100.

“Wanawekeza jumla ya dola bilioni 1.3 (shilingi trilioni 3.24) nimeongea nao waharakishe na wamekubali, hivyo mradi huu unachagiza ajenda ya kiuchumi ya nchi yetu” ameongeza prof. Mkumbo.

Profesa Mkumbo amebainisha kuwa, Uwekezaji huo ni matunda ya ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Indonesia mapema mwaka 2024 kama ilivyokuwa kwa ziara ya nchini Burundi iliyopelekea kujengwa kwa kiwanda kikubwa cha mbolea cha Itracom.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema hatua hiyo itasaidia kuokoa matumizi ya fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea nje ya nchi.

Laurent ameeleza kuwa, kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mbolea nchini kutoka tani laki tani laki tano kwa mwaka 2022/2023 na kufikia tani laki nane kwa mwaka 2023/2024 na matarajio ya kuongeza matumizi hadi kufikia tani milioni moja.

Mwisho Laurent ametoa wito kwa wakulima kuendelea kujisajili ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku zitakazoendelea kutolewa na serikali mpaka ifikapo mwaka 2025/2026.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri  akizungumzia  umuhimu wa uwekezaji huo amesema utazalisha ajira takribani laki nne tangu kuanza kwa mradi huo hadi kukamilika kwake.