Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA yazungumza na wawekezaji kuendeleza tasnia ya mbolea nchini
30 May, 2024
TFRA yazungumza na wawekezaji kuendeleza tasnia ya mbolea nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent ametumia ushiriki wake katika mkutano wa wadau wa mbolea wa Afriqom Fertilizer Club kuzungumza na wawekezaji walioshiriki mkutano huo kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.



Mazungumzo hayo yalilenga katika kuanzisha ushirikiano baina ya wawekezaji na Mamlaka ili kuendelea kuinua tasnia ya mbolea nchini.



Akizungumza na uongozi wa juu wa kampuni la mbolea la OCP Africa mkurugenzi Laurent ametoashukrani kwa uongozi wa juu wa OCP kwa namna kampuni hiyo inavyoshiriki kikamilifu katika kuhudumia wakulima kwa kuwafikishia mbolea pamoja na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea inayotolewa katika maeneo mbalimbali nchini.



"Tunaelewa kazi kubwa na nzuri sana mnayoifanya ya kusambaza mbolea kwa wakulima lakini pia kuwahamasisha kutumia mbolea tunawashukuru sana" Joel aliongeza.



Aidha, Laurent amewaomba wasambazaji wa mbolea nchini kuwa na imani na serikali katika kulipa gharama ya mbolea ya ruzuku ya mwaka 2022/2023 na kueleza mpaka sasa theluthi mbili ya deni lote imekwishalipwa na kiasi kilichobaki kitalipwa kupitia bajeti iliyotengwa kwa mwaka 2023/2024 wa fedha.



Ameeleza kuwa, kufuatia uwepo wa ruzuku ya mbolea kwa msimu uliopita wakulima walihamasika sana kutumia pembejeo hiyo kwenye kilimo na hivyo bajeti iliyotegwa kutotosheleza maana kiasi kilichotumika ni mara mbili ya bajeti iliyotengwa na kuwasihi kuwa na subra kwani malipo hayo ni lazima yafanyike.



Akizungumza katika kikao hicho Mohamed Hettit Makamu wa Rais wa kampuni la mbolea la OCP ameipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuja na mfumo wa kidigitali katika kusambaza mbolea.



Amesema, mfumo huo umekuwa namsaada mkubwa kwa wafanyabiashara kwani unasaidia katika kubaini mahitaji ya mbolea nchini kulingana na msimu pamoja na kurahisisha upatikanaji wa takwimu mbalimbali za mauzo.



Kwa siku mbili za mkutano mjini Zanzibar, Mkurugenzi Joel amefanya mahojiano na kampuni tofautitofauti ikiwa ni pamoja na AgroAmerican plc Group, Fertilizer Management and Handling Solutions (BAGTECH), Black Point Agriculture, Afriqom na United Fertilizer Company Limited kujadili namna pande hizo zitakavyoshirikiana katika kuendeleza tasnia ya mbolea nchini.