Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA YAWAJENGEA UWEZO WAZALISHAJI WA MBOLEA
29 May, 2024
TFRA YAWAJENGEA UWEZO WAZALISHAJI WA MBOLEA

Na Mwandishi wetu

WAZALISHAJI wa mbolea nchini wametakiwa kutumia fursa ya upatikanaji wa malighafi muhimu za kuzalisha mbolea kwa kuanzisha viwanda vyambolea na visaidizi vyake ili kukidhi mahitaji ya mbolea nchini.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wazalishaji wa mbolea nchini.

Dkt Ngailo amesema kuwa Tanzania ina akiba ya madini mbalimbali yakiwemo yale yanayotumika katika kuzalisha mbolea kama vile phospheti ambayo yanaongeza fursa kwenye uwekezaji wa kutengeneza mbolea hivyo, kumhakikishia mkulima uwepo wa mbolea bora za kutosha na kwa bei nafuu.

“Nawaomba mtumie fursa hii kuweza kuendeleza sekta ya mbolea kwa kuwekeza katika viwanda vya mbolea na visaidizi vyake ili kumhakikishia mkulima uwepo wa mbolea bora za kutosha na kwa bei nafuu,” alisema Dkt. Ngailo.

Amesema uzalishaji wa mbolea utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya ajira nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea amesema kuwa viwanda vya mbolea na visaidizi vyake vinakidhi mahitaji ya mbolea kwa asilimia tano tu ya mahitaji ya mbolea kwa mwaka ambayo ni tani 600,000 tu.

Amesema hali hiyo inatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa taarifa muhimu na za kutosha kuhusu uzalishaji wa mbolea na visaidi vyake na zinazohusiana na masuala ya uwekezaji.

“Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania imeandaa mafunzo haya mahsusi ili kujengeana uwezo na uelewa na kuwawezesha kutumia fursa kubwa iliyopo katika biashara ya mbolea ambapo kwa sasa takriban asilimia 90ya mbolea inatoaka nje ya nchi”, alisema Dkt Ngailo.

Amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza hamasa ya kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea wa ndani ya nchi na hivyo, kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea toka nje ya nchi.

Dkt. Ngailo ameongeza kuwa uzalishaji wa ndani pia utaimarisha urari wa biashara na mataifa ya nje (Balance of Trade), utaongeza ajira na kupunguza ucheleweshaji wa upatikanaji wa mbolea na kuongeza pato la ndani.

Mafunzo hayo yaliyowaleta pamoja wazalishaji wa mbolea, wauzaji na watendaji mbalimbali wa Serikali wanao husika na masuala ya viwanda, uratibu wa uingizaji wa mbolea kutoka nje nchi na watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini.

Mada zilizowasilishwa ni pamoja na Elimu ya Kemia na Biolojia ya Mbolea, Viwango vya Mbolea, Elimu ya Viwanda vya Mbolea, Nishati na Uwekezaji.

Mada zingine ni Elimu ya kwa Mlipa Kodi, Usalama Mahali pa Kazi na Wasilisho kutoka Kiwanda cha Kutengeneza Mbolea cha Mijingu na viwanda vya Sementi.

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ilianzishwa kwa Sheria namba 9 ya mwaka 2009 na kurekebishwa mwaka 2014 kwa lengo la kusimamia na kudhibiti ubora na biashara ya mbolea nchini. Mamlaka inasajili mbolea mpya, kutoa leseni na kutunza kumbukumbu za wauzaji wote wa mbolea nchini.

Vile vile Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania inatoa vibali vya utengenezaji, uagizaji na usambazaji wa mbolea nchini na kutoa miongozo mbalimbali ya usimamizi na udhibiti wa ubora na biashara ya mbolea.

MWISHO