Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA YATOA ELIMU MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA MIKOA YA KUSINI
29 May, 2024
TFRA YATOA ELIMU MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA MIKOA YA KUSINI

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara imetoa elimu kwa vitendo kupitia mashamba darasa kwa ajili ya kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya mahindi na mpunga.

Katika jitihada zake za kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwenye mikoa hiyo serikali kupitia TFRA imeanzisha mashamba darasa katika halmashauri za Ruangwa, Mtama, Mtwara na Masasi ambapo wakulima kupitia vikundi vyao wamepata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa njia ya vitendo.

Akitoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea katika halmashauri hizo, Afisa Udhibiti Ubora kutoka TFRA Aziz Mtambo amesema mkulima hawezi kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao shambani pasipo kutumia mbolea.

Mtambo amesema ili mmea ukue na kutoa mavuno bora shambani unahitaji virutubisho vya kutosha na virutubisho hivyo hupatikana kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha.

Ameongeza kuwa upungufu wa virutubisho unapotokea shambani huhitajika kuongezwa kwa kuweka mbolea ambayo amesema huwa na virutubisho mbalimbali ikiwemo naitrojeni, fosiforasi na potasiamu.

Mtaalamu huyo amesema kuwa mambo muhimu anayotakiwa kuzingatia mkulima kabla ya kuweka mbolea ni pamoja na afya ya udongo wa shamba, aina ya mbolea itakayotumika na upatikanaji wa mbolea husika.

Amesema matumizi sahihi ya mbolea ni lazima yazingatie kanuni bora zingine za kilimo ikiwemo kuandaa shamba kwa wakati, matumizi ya mbegu bora, kupalilia, kupiga madawa ya kuzuia na kuua wadudu na magonjwa mbalimbali na kuvuna kwa wakati unaostahili.

“Ni vema wakulima mkafahamu kuwa matumizi sahihi ya mbolea ni pamoja na kutumia mbolea sahihi, kiwango sahihi , wakati sahihi na sehemu sahihi ili kuleta matokeo mazuri yatakayoongeza tija katika uzalishaji wa mazao”, alisema Mtambo.

Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Kitere iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara Swalehe Tendwa amesema kupima afya ya udongo inasaidia kutambua virutubisho vilivyopo kwenye udongo na vipo kwa kiasi gani na uchachu uliopo.

Tendwa ameongeza kuwa faida za kupima afya ya udongo ni pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji kwani mkulima atanunua mbolea kulinganana upungufu uliopo kwenye udongo wa shamba lake na kutambua kiwango sahihi cha mbolea kinachohitajika.

Aidha amesema uhamasishaji wa matumizi ya mbolea unaofanywa na TFRA kwa kushirikiana na mikoa ya Lindi na Mtwara umeleta mwamko mkubwa kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo ambapo wananchi wengi wamekuwa wakipita katika mashamba darasa hayo ili kujifunza faida za kutumia mbolea katika uzalishaji wa mpunga na mahindi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashamba darasa hayo hivi karibuni alisema kuanzishwa kwa mashamba hayo kutaleta hamasa kubwa kwa wakulima wa mikoa hiyo kutaka kutumia mbolea katika uzalishaji wa mazao mbalimbali na hivyo kuongeza kipato.

Amesema mikoa ya Lindi na Mtwara ina zaidi ya hekta 6,400, 000 zinazofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali, hata hivyo tija ya uzalishaji kwenye mazao mengi bado ni ndogo.