Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA YATEMBELEA KIWANDA CHA MBOLEA YA ASILI MABWEPANDE
17 Oct, 2026
TFRA YATEMBELEA KIWANDA CHA MBOLEA YA ASILI MABWEPANDE

Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wametembelea Kiwanda cha Mabwepande Compost Management Limited kilichopo Bunju jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani inayoadhimishwa Oktoba 13 ya kila mwaka.

Akieleza lengo la ziara hiyo, Meneja wa TFRA Kanda ya Mashariki, Daniel Maarifa amesema ni juhudi za Mamlaka katika kuhamasisha  uzalishaji wa mbolea nchini kupitia rasilimali zilizopo ambapo taka zinazooza ni miongoni mwa fursa hiyo pamoja na utunzaji wa mazingira.

Akisoma taarifa ya mradi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mtaalamu wa Uzalishaji wa Mbolea ya Asili katika kiwanda hicho, Jimson Mkenda amesema kuwa mradi wa uzalishaji wa mbolea  asilia wa Mabwepande unatekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa ufadhili wa Jiji la Hamburg nchini Ujerumani, kupitia Serikali ya Tanzania, kwa gharama ya Sh bilioni 6.3, huku bajeti ya jumla ya mradi ikiwa Sh bilioni 7.91.

Alisema mradi huo hupokea taka zinazooza kutoka masoko sita yaliyopo katika halmashauri nne za Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo taka za matunda na bidhaa nyingine hupatikana kwa wingi huku uendeshaji wake ukichangiwa pia na Manispaa ya Kinondoni.

Mkenda amesema hadi sasa mradi huo umefanikiwa kuuza takribani kilogramu milioni 1.4 za mbolea, huku mipango ya kununua makontena zaidi ili kufikisha huduma katika masoko mengi na kuongeza ukusanyaji wa taka zinazooza ikiendelea . 

Amesema kiwanda chake  kitaendelea kutoa elimu ya ukusanyaji wa taka hizo ili wananchi wawe na utamaduni wa kutenganisha taka zinazooza na zisizooza ili kuweka jiji safi, kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

Kwa upande wake, Meneja wa Maabara ya TFRA, Leila Robin amesema lengo la Mamlaka kutembelea kiwanda hicho ni   pamoja na kujionea shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo na kutoa rai kwa wazalishaji wa mbolea za asili nchini kuhakikisha mbolea zote wanazozalisha zinapimwa maabara kabla ya kumfikia mlaji au kutumika ili kuthibitisha ubora na kiwango cha virutubisho vilivyopo. 

Aliwahimiza wazalishaji  kupeleka mbolea zao maabara ili kubaini kiwango cha madini tembo kwenye mbolea hizo, ambayo huwa na madhara kwenye afya ya mlaji.  

Naye, Meneja wa Uhamasishaji wa Uzalishaji wa Mbolea na Mazingira wa TFRA, Getrude Ng’weshemi amesema Mamlaka inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea na kufuatilia maendeleo ya viwanda vilivyowekeza nchini ili kuhakikisha vinazalisha mbolea yenye ubora.