Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA yatakiwa kutathimini manufaa ya mbolea ya ruzuku
29 May, 2024
TFRA yatakiwa kutathimini manufaa ya mbolea ya ruzuku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufanya tathimini ya manufaa ya ruzuku ya mbolea iliyotolewa kwa wakulima kwa mwaka 2022/2023.



Ameitaka kuhusianisha kiasi cha mbolea kilichofikishwa kwa wakulima na hali ya uzalishaji ili kujiridhisha endapo mbolea imetumika katika mashamba ya wakulima na hivyo kuongeza tija kwenye uzalishaji au vinginevyo.



Rais, Dkt. Samia ametoa wito huo leo alipotembelea banda la Mamlaka ikiwa ni siku ya kilele cha sikukuu ya wakulima maarufu kama nanenane yaliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.



Amesema mbolea ikisambazwa kwa wakulima na isioneshe matokeo yenye tija italeta maswali mengi lakini kukiwa na takwimu zinazoonesha kiasi cha mbolea kilichowafikia wakulima na kiasi cha mazao yaliyopatikana baada ya kutumia mbolea itaonesha dhahiri kuwa kazi inayofanywa ni nzuri.



"Atleast nione ongezeko kwenye uzalishaji" Dkt. Samia alisisitiza



Kwa upande wake, Waziri wa kilimo Hussein Bashe amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa mbolea za ruzuku kwa msimu wa kilimo 2022/2023 na kuendelea kwa msimu huu wa 2023/2024.



Ameeleza kuwa, tathimini ya awali iliyofanyika imeonesha ongezeko la uzalishaji kutoka junia moja bila kutumia mbolea mpaka junia tisa baada ya kutumia mbolea kwa ekari moja.



Waziri Bashe amesema, kiasi cha shilingi bilioni 200 kimetegwa kugharamia ruzuku ya mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024 huku matumizi kwa msimu huu wa kilimo yakikadiriwa kuwa tani laki sita na nusu (650,000)



Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo ameeleza kuwa, matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani laki tatu na sitini na tatu (363,000) kwa msimu wa kilimo wa 2021/2022 na kufikia tani laki tano na elfu themanini (tani 580,000) msimu wa kilimo 2022/2023 huku tani laki tatu na themanini (380,000) zikinunuliwa kwa mfumo wa ruzuku na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 368.



Aidha, Dkt. Ngailo ameahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Rais, Dkt. Samia ikiwa ni pamoja na kutathmin manufaa ya mbolea za ruzuku kwa wakulima.

Mbolea Day