Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

TFRA yapongezwa usimamizi mzuri mbolea za ruzuku


Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa ameipongeza Serikali kwa kuja na mfumo wa utoaji wa mbolea za ruzuku na kueleza zimeleta mwamko kwa wakulima na kuongeza uzalishaji.

"Serikali imekuja na mpango mzuri tunaufurahia kwani mbolea zinafika kwa walengwa hasa tofauti na mifumo iliyopita ambapo wachache walijinufaisha" Mwassa aliongeza.

Mkuu wa Mkoa, Mwassa ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania waliofika ofisini kwake kueleza lengo la ziara yao mkoani humo

Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo amesema, ziara hiyo imelenga kutoa hamasa kwa viongozi wa mikoa kuwasimamua kikamilifu maafisa ugani wa maeneo hayo kutoa taarifa sahihi za matumizi ya mbolea ili kusaidia kuwa na takwimu sahihi zitakazosaidia wakulima kufikishiwa pembejeo hiyo kwa wakati na kwa utoshelevu.

Aidha, Mwenyekiti Dkt. Diallo, ameuomba uongozi wa Mkoa wa Kagera kufuatilia matumizi ya vifaa vya kupimia afya ya udongo vilivyotolewa na serikali kwa maafisa Ugani ili kusaidia kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya udongo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent ameushukuru uongozi wa Mkoa kwa jitihada wanazochukua za kuhamasisha usajili wa wakulima na matumizi ya mbolea.

Amewahakikishia kuwa, Mamlaka itaendelea kusimamia ubora wa mbolea na kuhakikisha inamfikia mkulima karibu na shamba lake pamoja na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija katika uzalishaji wao