Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji mbolea: Prof. Mkenda


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Kilimo, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali ipo kwenye mikakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa kittovu cha kuingiza mbolea na kusambaza kwa nchi jirani zenye uhitaji.

Ameyasema hayo tarehe 14 Juni 2021 wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia shughuli ya upakuaji na uingizaji wa mbolea ndani ya nchi.

Prof. Mkenda amesema njia mojawapo ya kuhakikisha mbolea inashuka ni kuhakikisha mbolea nyingi inaingia nchini, na ili kufanikisha hilo lazima Tanzania iwe ni “kitovu cha kuagiza na kuingiza mbolea katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendelea Kusini mwa Afrika (SADC).

“Kwa bahati mbaya hivi karibuni Zambia walikuwa wanaleta mbolea kupitia bandari yetu lakini kwa sasa wanaleta kupitia bandari nyingine, tunataka warudi waingize mbolea kupitia bandari ya Dar es Salaam.

“Tunapenda wafanyabiashara walete mbolea kwa wingi hapa nchini, sisi tutaweka mfumo mzuri wa kuwarahishia kuiondoa mapema ili kuipeleka Congo na Zambia au nchi nyingine yoyote wanapotaka kwenda kuuza, “Amesema.

Waziri amesema kuwa hiyo ni hatua ya awali, nyingine wanatarajia kuimarisha uzalishaji wa mbolea ili kufanikisha kupatikana kwa wingi nchini.

“Kuna kiwanda kikubwa cha mbolea kinajengwa Dodoma, yule wa Minjingu tumemwambia tutamlinda na aongeze ufanisi wa mbolea yake ili kazi iende mbele, hii itatusaidia sisi wakulima kupata mbolea kwa bei nafuu, hivyo mazao yatauzwa pia kwa bei rahisi,” alisema Profesa Mkenda.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda hatua hiyo inalenga katika kuongeza ushindani wa kuingiza mbolea nchini na hiyo ndiyo sababu ya kuongeza muda wa zabuni ili kuwe na kampuni nyingi ambazo zitakuja kushindana kuleta mbolea.

Kuhusu bei ya mbolea, Waziri Mkenda amesema kuwa, kwa sasa inaongezeka duniani na hata hapa nchini imeshapanda ambapo kati ya Juni 2020 na Juni 2021 bei imeongezeka kwa asilimia 50.

“Mahitaji ya mbolea nchini ni takribani tani laki saba kwa mwaka , wakati uzalishaji wetu ni tani chini ya laki moja, tayari tumeanza mazungumzo na mwakilishi wa ubalozi wa Saudi Arabia na Qutar.

Nchi hizo, amesema Profesa Mkenda ni mojawapo ya nchi ambazo zinazalisha mbolea kwa wingi, na ameahidi kuendelea kufanya mazungumzo na mabalozi wengine kuwashawishi ili makampuni yaliyoko nchini mwao kuja kuwekeza nchini na hii itachangia bei zipungue,”Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo amesema kuwa suala la vibali wameshaanza kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanaoomba vibali wanapatiwa kwa wakati.

“Tunatarajia kuanza kuruhusu wafanyabiashara kuomba vibali vya kuingiza mbolea wanapata hati ya kulipia kwa njia ya mtandao na kibali pia.

Amesema utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao itarahisisha vibali kutolewa kwa wakati, hivyo itaongeza ufanisi kwani lengo ni kuona kuwa mkulima anapata mbolea bora, kwa bei nafuu na kwa wakati uliokusudiwa.

Akizungumza mapema, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema amemueleza Waziri Mkenda kuwa TFRA imeboresha mfumo wa upakiaji wa mbolea unaofanywa kwa njia ya kisasa unaowezesha upakiaji kufanyika haraka.

Bw. Lema amesema kuwa mashine ya awali ilikuwa na uwezo wa kupakia mifuko 1, 500 kwa saa 24 lakini mashine ya ya kisasa ina uwezo wa kujaza mifuko 3000.

Mwisho.

Tanzania Census 2022