Tanzania kuwa kitovu cha mbolea ifikapo 2030

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo amesema, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea ya urea unaotarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya ESSA ya nchini Indonesia, ni hatua muhimu ya kufikia maono ya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa mbolea Afrika Mashariki na Kati.
Dkt.Diallo amesema hatua hiyo inakwenda sambamba na kutatua changamoto zinazolikabili soko la mbolea nchini.
Dkt. Diallo ametoa kauli hiyo leo, tarehe 19 Mei 2025, katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya awali ya mauziano ya gesi kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya ESSA Industries, iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa, kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikitegemea mbolea kutoka nje ya nchi, jambo ambalo limesababisha matumizi makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza pembejeo hiyo muhimu kwa kilimo.
“Kujengwa kwa kiwanda hiki kutapunguza utegemezi wa mbolea ya uagizaji, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu,” amesema Dkt. Diallo.
Ameongeza kuwa viwanda vingi vya ndani vinategemea mbolea ya urea kama malighafi, hivyo upatikanaji wake wa uhakika kupitia uzalishaji wa ndani utakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kilimo na viwanda nchini.
Dkt. Diallo amesisitiza kuwa, kwa kutumia rasilimali ya gesi asilia, Tanzania sasa ipo katika nafasi nzuri ya kuzalisha mbolea ya urea kwa wingi, hatua itakayosaidia kuimarisha usambazaji wa mbolea sokoni, kupunguza gharama kwa wakulima na kuleta ustawi wa uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya ESSA, Bw. Rahul Puri ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano uliowezesha hatua ya awali ya makubaliano ya mauziano ya gesi, na kueleza kuwa hatua inayofuata ni kufanya utafiti wa kina kuhusu kiasi cha gesi kitakachohitajika kwa uzalishaji wa mbolea.
Amebainisha kuwa, ushirikiano kati ya TFRA, TIC, TFC na TPDC ndio msingi wa mafanikio ya uwekezaji huo unaotarajiwa kugharimu takribani Dola za Marekani bilioni 1.4 na kukamilika ifikapo mwaka 2030.
Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa TPDC, Bw. Derick Moshi amesema shirika hilo litaendelea kuhakikisha upatikanaji wa gesi kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea unakuwa wa uhakika, huku likiwa mbia muhimu katika kuhakikisha malengo ya uwekezaji huo yanafikiwa.
Kwa upande wake, Bw. Lameck Borega kutoka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), amesema mradi huo una faida kubwa kwa nchi, ikiwemo kuongez