Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
SERIKALI YATOA MB0LEA YA RUZUKU ZAIDI YA TANI MILIONI 1,454,974.721 KWA MIAKA MITATU
21 May, 2025
SERIKALI YATOA MB0LEA YA RUZUKU ZAIDI YA TANI MILIONI 1,454,974.721 KWA MIAKA MITATU

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohamed Bashe amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2024/2025, serikali imetoa mbolea ya ruzuku yenye jumla ya tani 1,454,974.721 yenye thamani ya Shilingi 708,627,762,436 kwa wakulima wa mazao yote nchini.

Mhe. Bashe ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango wa ruzuku umechangia ongezeko kubwa la matumizi ya mbolea kutoka tani 363,599 mwaka 2021/2022 hadi tani 848,884 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 133.47.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 21 Mei, 2025 Bungeni Jijini Dodoma akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka 2025/2026 ya shilingi trilioni 1.24.

Aidha, Waziri Bashe amesema, uzalishaji wa ndani wa mbolea umeongezeka kutoka tani 32,230 mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 158,628 mwaka 2024/2025, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 392.

Ameeleza kuwa, mafanikio hayo yamechangiwa na kuanzishwa kwa kiwanda cha Itracom kilichopo Nala, Jijini Dodoma pamoja na upanuzi wa kiwanda cha Minjingu, ambacho kimeongeza uwezo wake wa uzalishaji kutoka tani 30,000 hadi 100,000 kwa mwaka.

Amesema, kutokana na ongezeko la uzalishaji, upatikanaji wa mbolea umeimarika kutoka tani 678,017 mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 1,213,729 mwaka 2024/2025, ongezeko la asilimia 79.

Pia, Waziri Bashe amebainisha kuwa, matumizi ya mbolea kwa hekta yameongezeka kutoka kilo 19 mwaka 2021/2022 hadi kilo 24 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 26.

Kuhusu urasimishaji wa wakulima wadogo, Waziri Bashe amesema, serikali ilipanga kurasimisha wakulima 10,000 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kuwapatia hati za hakimiliki za ardhi na kubainisha kuwa, hadi Aprili, 2025  Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi wamepima jumla ya mashamba ya wakulima 9,117 walikuwa wamepimiwa ardhi na kupatiwa hati za hakimiliki za ardhi katika halmashauri za Iramba (Singida), Mbinga (Ruvuma), Songwe (Songwe), na Chamwino (Dodoma).

Akizungumzia usajili wa wakulima na wadau wengine wa pembejeo, Waziri Bashe amesema hadi sasa wakulima 4,522,011 wamesajiliwa kwenye mfumo wa Pembejeo za Kilimo. Aidha, waagizaji wa mbolea 64, wasambazaji 7,147 na vyama vya ushirika 720 tayari vimesajiliwa ili kurahisisha usambazaji wa pembejeo kwa wakulima nchini.